Jun 11, 2022 02:34 UTC
  • Magaidi 800 wa Boko Haram wauawa katika eneo la Ziwa Chad

Mamia ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameangamizwa katika operesheni za Vikosi vya Pamoja vya Kimataifa (MNJTF) katika eneo la Ziwa Chad, magharibi mwa Afrika.

Hayo yamesemwa na Jenerali Abdul Kalifa Ibrahim, Kamanda Mkuu wa vikosi hivyo vya pamoja na kueleza kuwa, magaidi 800 wa Boko Haram wameuwa katika operesheni hiyo iliyopewa jina la 'Lake Sanity' iliyofanyika ndani ya siku 75 zilizopita.

Jenerali Ibrahim ameongeza kuwa, magaidi hao wameangamizwa kutokana na ushirikiano wa karibu wa wanajeshi kutoka nchi za Cameroon, Nigeria, Chad na Niger.

Kamanda huyo amebainisha kuwa, "katika operesheni hii iliyofanyiwa kwa takriban miezi mitatu, hakuna askari hata mmoja wa Cameroon ameuawa, hii ni rekodi ya aina yake."

Amesema vikosi hivyo vya pamoja vya kieneo vimefanikiwa kukamata pia vifaa kadhaa vya magaidi hao, zikiwemo silaha, mada za miripuko na zana zingine za kijeshi.

Ramani inayoonesha nchi za eneo la Ziwa Chad

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa, limewaangamiza magaidi wapatao 40 wa kundi la Boko Haram katika visiwa vya Ziwa Chad lililoko kwenye mpaka wa pamoja wa Nigeria, Niger, Cameron na Chad.

Hujuma na mashambulio ya  Boko Haram yameshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad, tokea mwaka 2009.

Tags