Jun 14, 2022 08:04 UTC
  • Watu zaidi ya 100 wauawa katika shambulio la waasi Burkina Faso

Serikali ya Burkina Faso imetangaza kuwa watu wasiopungua 50 wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika kijiji kimoja kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Lionel Bilgo, washambuliaji hao walishambulia usiku wa kuamkia Jumapili katika kijiji cha Seytenga ambacho kiko katika mkoa wa Seno ulioko maeneo ya mpakani ambako wanamgambo wenye mfungamano na magenge ya kigaidi ya Al Qaeda na DAESH (ISIS) wanahusika na mashambulio ya kutumia silaha.

Bilgo amefafanua kuwa hadi sasa jeshi limepata maiti za watu 50 baada ya kijiji cha Seytenga kushambuliwa Jumamosi usiku na kuongeza kuwa idadi ya vifo "inaweza kuongezeka".

Lakini mbali na takwimu zilizotolewa na msemaji wa serikali ya Burkina Faso, afisa mmoja wa usalama amevieleza vyombo vya habari kuwa watu wasiopungua 100 wameuawa huku raia mmoja katika eneo la tukio ambaye hakutaka kutajwa jina lake akisema watu wapatao 165 wameuliwa katika hujuma hiyo.

Umoja wa Mataifa umelaani shambulio hilo ambalo umesema "limesababisha maafa ya roho za watu wengi" na kuzitolea mwito mamlaka husika za Burkina Faso kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya sheria.

Roch Marc Christian Kabore

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, naye pia amelaani mauaji hayo na kutaka ufanyike ufuatiliaji wa kubainisha wazi namna mauaji hayo yalivyofanywa.

Wiki iliyopita, eneo la Seytenga ulikuwa uwanja wa mapigano makali ya umwagaji damu kati ya waasi na vikosi vya serikali.

Siku ya Alkhamisi, askari polisi 11 waliuawa na kupelekea kutekelezwa operesheni ya kijeshi ambayo kwa mujibu wa jeshi la Burkina Faso ilipelekea kuuawa waasi wapatao 40.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Bilgo, umwagaji damu uliofanywa dhidi ya raia wa Seytenga umetokana na kisasi kilicholipizwa kutokana na hatua zilizochukuliwa na jeshi.

Jumuiya zinazotoa huduma za kibinadamu nchini Burkina Faso zimesema  watu wapatao elfu tatu wanapatiwa makazi kwenye miji ya jirani baada ya kukihama kijiji cha Seytenga.

Shambulio la Jumamosi ni moja ya hujuma kubwa zaidi za umwagaji damu kutokea nchini Burkina Faso tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi mwezi Januari, yaliyomwondoa madarakani rais Roch Marc Christian Kabore, baada ya makanali wa jeshi la taifa kukasirishwa na kile walichodai kushindwa serikali yake kuyasambaratisha makundi ya wabeba silaha.../

Tags