Algeria yasimamisha uhusiano wa kitalii na Uhispania, mvutano washtadi
(last modified Tue, 21 Jun 2022 07:51:56 GMT )
Jun 21, 2022 07:51 UTC
  • Algeria yasimamisha uhusiano wa kitalii na Uhispania, mvutano washtadi

Serikali ya Algeria imetangaza kusimamisha uhusiano wa kitalii wa nchi hiyo na Uhispania, huku mzozo baina mataifa hayo mawili juu ya mgogoro wa Sahara Magharibi ukiongezeka.

Wizara ya Utalii ya Algeria imeyaagiza mashirika yote ya kitalii nchini humo kusimamisha mara moja uhusiano wao na Uhispania, ikisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uamuzi wa serikali ya Algiers kusimamisha mkataba wa urafiki na Madrid.

Mapema mwezi huu pia, Algeria ilichukua hatua "mara moja" kusimamisha mkataba wa urafiki baina yake na Uhispania baada ya Madrid kubadilisha msimamo wa miongo kadhaa wa kutoegemea upande wowote katika mgogoro wa Sahara Magharibi.

Uamuzi huo wa Algeria ni pigo jipya kwa uhusiano unaozidi kulegalega wa Algiers na Madrid, ambayo inaitegemea Algeria kwa ajili ya nishati ya gesi asilia.

Mzozo baina ya nchi mbili hizi ulishtadi mwezi Machi mwaka huu, baada ya serikali ya Madrid kutangaza kuwa inasimama upande wa Morocco juu ya eneo lenye mgogoro la Sahara Magharibi. Algeria ilimwita nyumbani balozi wake wa Uhispania kwa ajili ya mashauriano, kutokana na msimamo huo wa Madrid.

Wakazi wa eneo la Sahara Magharibi katika maandamano

Algeria inasisitiza kuwa,  Uhispania inaharibu nafasi yake ya "mamlaka ya uendeshaji" katika Sahara Magharibi inayopasa kuwa nayo hadi pale Umoja wa Mataifa utakapotatua mgogoro wa miongo kadhaa kuhusu hatima ya eneo hilo lenye utajiri wa madini.

Kwa sasa, Morocco inadhibitii asilimia 80 ya eneo la Sahara Magharibi huku sehemu iliyosalia ikishikiliwa na Harakati ya Polisario inayoungwa mkono na Algeria. Kwa miaka 15, Polisario imepigana vita na Morocco vya kulikomboa eneo hilo, baada ya Uhispania kuondoa askari wake mwaka 1975 na inataka iitishwe kura ya maoni ya kuamua uhuru na kujitawala watu wa Sahara Magharibi.