Libya yapinga uingiliaji kijeshi wa madola ya kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8503-libya_yapinga_uingiliaji_kijeshi_wa_madola_ya_kigeni
Waziri Mkuu wa Libya amepinga uingiliaji wa kijeshi nchini humo ambao umekuwa ukipangwa na baadhi ya madola kwa kisingizio cha kupambana na magaidi wa ISIS nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2016 03:03 UTC
  • Libya yapinga uingiliaji kijeshi wa madola ya kigeni

Waziri Mkuu wa Libya amepinga uingiliaji wa kijeshi nchini humo ambao umekuwa ukipangwa na baadhi ya madola kwa kisingizio cha kupambana na magaidi wa ISIS nchini humo.

Fayez al Sarraj katika mahojiano na jarida la Kifaransa Le Journal du Dimanche amesema, "Ni kweli tunahitaji msaada wa jamii ya kimataifa katika vita dhidi ya ugaidi na ni kweli tayari tumeshaanza kupokea misaada."

Hata hivyo amesema Libya haitaki vikosi vya kigeni viingie nchini humo kwani jambo hilo ni kinyume cha misingi ya taifa hilo. Amesema nchi yake inahitajia picha za satalaiti, habari za kiintelijensia na misaada ya kiufundi na si ndege za kivita za kigeni zidondeshe mabomu nchini humo.

Sarraj ameongeza kuwa, jeshi la Libya hivi sasa linakaribia kupata ushindi dhidi ya magaidi wa ISIS katika mji wa Sirte. Amebainisha matumaini yake kuwa vita dhidi ya ugaidi vitawaunganisha Walibya na kuongeza kuwa vita hivyo vitadumu muda mrefu.

Siku ya Jumamosi vikosi vya serikali ya Libya vilichukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa kijeshi wa Ghardabiya yapata kilomita 20 kusini mwa Sirte.