Tahadhari ya UN kuhusu kusitishwa misaada ya kibinadamu Somalia
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kuhusu kusimamishwa misaada ya kibinadamu nchini Somalia.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilitangaza katika ripoti yake hivi majuzi kwamba Somalia inakabiliwa na njaa isiyo na kifani katika miaka 40 iliyopita.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imetangaza kwamba, ikiwa jamii ya kimataifa haitatuma msaada haraka nchini Somalia, shirika hilo la kimataifa litalazimika kusitisha mipango yake ya misaada kwa Wasomali kutokana na ukosefu wa fedha.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa bila ufadhili wa haraka, programu za misaada kama vile chakula, lishe na huduma za afya zitasitishwa, na Wasomali zaidi watakuwa wahanga wa njaa na ukame.
OCHA imeonya kwamba ukame mkubwa nchini Somalia umeathiri watu milioni 7.7, ambao ni karibu nusu ya wakazi wa nchi hiyo na kwamba wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu au ulinzi.
Ripoti zinasema maelfu ya watu nchini Somalia wameacha makazi yao na kukimbilia katika kambi za wakimbizi kutafuta msaada wa chakula.
Wataalamu wanasema, ukame na mabadiliko ya hali ya hewa umesababisha hasara ya mifugo na njaa kubwa katika maeneo mengi ya Pembe ya Afrika.