Hofu ya AU, IGAD kuhusu mapigano mapya Tigray, Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i87416-hofu_ya_au_igad_kuhusu_mapigano_mapya_tigray_ethiopia
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema ametiwa wasiwasi na ripoti za kuibuka makabiliano mapya ya kijeshi nchini Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 25, 2022 12:03 UTC
  • Hofu ya AU, IGAD kuhusu mapigano mapya Tigray, Ethiopia

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema ametiwa wasiwasi na ripoti za kuibuka makabiliano mapya ya kijeshi nchini Ethiopia.

Katika taarifa, Moussa Faki Mahamat amezitaka pande hasimu katika mgogoro wa eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia kujizuia na hatua zitakazoshadidisha hali ya mambo, na watafute ufumbuzi kwa njia za amani.

Mapema jana Jumatano, serikali ya Ethiopia iliwatuhumu wapiganaji wa Tigray People's Liberation Front (TPLF) kwa kuendeleza mapigano, licha ya kuwepo jitihada za kufanyika mazungumzo baina ya pande mbili ya kujaribu kutatua mzozo uliopo.

Wakati huohuo, Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Mashariki mwa Afrika na pembe ya Afrika IGAD imezitaka pande husika kujiepusha mara moja na hatua za kiuhasama zinazoweza kupelekea hali ya mambo kuwa mbaya zaidi.

Katibu Mkuu wa IGAD, Workneh Gebeyehu amesema mapigano mapya yaliyoripotiwa katika eneo la Tigray yanatia wasiwasi mkubwa, na amezitaka pande husika kutoa kipaumbele kwa mazungumzo.

Ramani inayoonesha eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia

Tangu mwezi Novemba mwaka juzi (2020) jimbo la Tigray limekumbwa na hitilafu na mivutano ya kisiasa kati ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na viongozi wa eneo hilo ambao wakati fulani waliongoza serikali ya Ethiopia.

Vita vilivyoshuhudiwa katika eneo hilo hadi sasa vimesababisha kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.