Mripuko wa kipindupindu waua makumi ya watu Kongo DR
(last modified Thu, 01 Sep 2022 07:34:09 GMT )
Sep 01, 2022 07:34 UTC
  • Mripuko wa kipindupindu waua makumi ya watu Kongo DR

Mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu umepelekea watu wasiopungua 48 kupoteza maisha katika mkoa wa Sankuru, katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vyombo vya habari vimewanukuu maafisa wa afya wakisema kuwa, mbali na vifo 48, kesi 401 ya maradhi hayo zimeripotiwa baina ya Agosti 15 na 21 mwaka huu.

Habari zaidi zinasema kuwa, zoni ya Lusambo ndiyo iliyosajili idadi kubwa ya vifo na kesi za ugonjwa huo, ambapo mbali na kuandikisha vifo 24, imerekodi pia kesi 308.

Mkuu wa Idara ya Afya katika mkoa wa Sankuru, Dakta Aimé Alengo amesema wameanzisha kampeni wakishirikiana na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef, vyombo vya habari, na makanisa ili kuwahamasisha watu jinsi ya kujiuzuia kupata maradhi hayo.

Watoto ni miongoni mwa waathirika wa kipindupindu DRC

Maafisa wa afya katika mkoa huo wametahadharisha kuwa, huenda watu wengi zaidi wakafariki dunia kwa kukosa huduma za msingi za afya hasa katika eneo hilo.

Mkoa wa Sankuru unakabiliana pia na magonjwa megine kama ukambi (surua), Homa ya Ndui (Monkeypox), matatizo ya kupumua na homa ya uti wa mgongo.

Tags