Ethiopia yakubali mwito wa AU wa kufanya mazungumzo na TPLF
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i88936-ethiopia_yakubali_mwito_wa_au_wa_kufanya_mazungumzo_na_tplf
Serikali ya Ethiopia kwa mara nyingine tena imesema imeafiki mwito wa Umoja wa Afrika (AU) wa kufanya mazungumzo ya amani na waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 06, 2022 03:10 UTC
  • Ethiopia yakubali mwito wa AU wa kufanya mazungumzo na TPLF

Serikali ya Ethiopia kwa mara nyingine tena imesema imeafiki mwito wa Umoja wa Afrika (AU) wa kufanya mazungumzo ya amani na waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Redwan Hussein, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter na kusisitiza kuwa: Serikali imekubali mwaliko huu unaoenda sambamba na msimamo na sera zetu.

Amefafanua kuwa, serikali ya Ethiopia ilishasema huko nyuma kwamba, ipo tayari kufanya mazungumzo na waasi hao bila ya masharti na wakati wowote na mahali popote.

Idara ya Mawasiliano ya Ethiopia bila kutoa maelezo ya kina imesema katika taarifa kuwa, AU imeshaainisha tarehe na mahala pa kufanyika mazungumzo hayo. Baadhi ya duru za habari zinasema mazungumzo hayo yatafanyika Afrika Kusini.

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia

Waasi wa eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia wamesema pia wanaafiki mchakato wa kusaka amani na serikali ya Addis Ababa chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika (AU).

Huku nyuma walikubali pia mwito wa mazungumzo, lakini walikosoa ukaribu uliopo kati ya mpatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) raia wa Nigeria, Olusegun Obasanjo na Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia.

Hadi sasa ikiwa imepita karibu miaka miwili ya vita katika eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia, maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.