Wanamgambo wa ADF waua watu 10 karibu na Uganda
(last modified Thu, 06 Oct 2022 03:23:56 GMT )
Oct 06, 2022 03:23 UTC
  • Wanamgambo wa ADF waua watu 10 karibu na Uganda

Kwa akali watu 10 wameuawa katika shambulizi jipya la waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, karibu na mpaka wa Uganda.

Patrick Musubao, kiongozi wa asasi moja ya kiraia katika mkoa huo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mbali na watu 11 kuuawa katika hujuma hiyo, wengine zaidi ya 20 hawajulikani walipo.

Amesema watu hao akiwemo mchungaji wa kanisa la Kianglikana waliuawa usiku wa kuamkia jana Jumatano, baada ya wanachama wa genge hilo kushambulia kijiji cha Vido, karibu na mpaka wa Uganda.

Naye Didi Isaya, afisa wa serikali katika mkoa wa Kivu Kaskazini sambamba na kuthibitisha kutokea mauaji hayo, amesema wanamgambo hao wameteketeza kwa moto nyumba zaidi ya 25 za wakazi wa kijiji hicho.

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

Vikosi vya Jeshi la Uganda (UPDF) na  Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vilianzisha mashambulizi mwaka jana ili kuwaondoa waasi hao wa ADF, ambao wamekuwa wakiwashambulia na kuwaua raia mashariki kwa zaidi ya miongo miwili.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, watu wasiopungua 40 waliuawa katika wimbi la mashambulizi yaliyofanywa na kundi hilo la kigaidi katika mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Tags