Jun 10, 2016 14:06 UTC
  • Zuma akata rufaa kupinga kufufuliwa kesi za ufisadi dhidi yake

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuagiza kufufuliwa kesi zaidi ya 700 za ufisadi wa kifedha dhidi yake.

Ofisi ya Zuma imesema kuwa, Mahakama Kuu ilikosea kutoa uamuzi wa kufufuliwa kesi 783 za ufisadi dhidi ya rais huyo, licha ya kuwa zilikuwa zimebatilishwa huko nyuma na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma. Taarifa ya ofisi ya rais iliyotolewa leo Ijumaa baada ya kufungua kesi hiyo ya rufaa imesema kuwa, uamuzi wa Mahakama Kuu ya Pretoria wa kutaka mrundiko wa kesi za ufisadi wa kifedha dhidi ya Zuma uangaliwe upya, hauna mantiki na kwamba ni kosa kudai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma hakuwa na mamlaka ya kutengua kesi hizo. Mwishoni mwa mwezi wa Aprili mwaka huu, Mahakama Kuu ya mjini Pretoria ilisema kuwa, uamuzi uliotolewa mwaka 2009 wa kutupilia mbali kesi zilizohusu madai ya ufisadi dhidi ya Rais Zuma, haukuwa na mantiki na kwa msingi huo, kesi hizo zinafaa kusikilizwa upya. David Borgstrom, wakili wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance amesema uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ni sahihi na kesi hizo dhidi ya Zuma zinafaa kusikilizwa upya. Haijabainika kesi hiyo ya rufaa itachukua muda gani. Tuhuma hizo zinahusiana na ununuzi tata wa silaha uliogharimu mlipa kodi mabilioni ya dola mwaka 1999 kutoka shirika moja la Ufaransa.

Tags