Oxfam: Ukame unatishia maisha ya maelfu ya watu barani Afrika
Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limetangaza kuwa, ukame barani Afrika huenda ukaua maelfu ya watu katika siku za usoni.
Oxfam ambalo ni shirika kubwa zaidi la kimataifa la misaada ya kutokomeza umaskini, inasema: Uhaba wa chakula yumkini ukasababisha kifo cha mtu mmoja kila baada ya sekunde 36 hadi kufikia mwisho wa mwaka huu.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kibinadamu yanayofanya kazi barani Afrika yamesema katika ripoti yao ya hivi karibuni kuhusu hali ya kimaisha ya watu wa bara hilo kwamba kuna udharura wa kuzidishwa misaada ya kibinadamu kwa nchi za Afrika.
Kulingana na ripoti hiyo, watu wa nchi kama Kenya, Somalia na Ethiopia wanakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka 40 iliyopita na wanahitaji msaada wa haraka.
Etienne Peterschmidt, mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, nchini Somalia amesema: "Hatupaswi kusubiri tangazo la njaa, kwa sababu wakati huo tutakuwa tayari tumechelewa."

Misimu minne mfululizo ya mvua duni imesababisha uharibifu wa mifugo na mazao, huku wakazi wa vijijini katika maeneo ya mbali ya Somalia wakiathirika zaidi.
Peterschmidt amesema, ukame wa sasa haujawahi kutokea katika miongo minne iliyopita na kwa sasa unaathiri karibu watu milioni 8. Amesema: Takriban nusu ya wakazi wa Somalia wanakabiliwa na njaa, na asilimia 90 ya watu wanasumbuliwa na hali ya ukame.
Ikumbukwe pia kwamba vita vya Ukraine na vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia vimevuruga usambazaji wa ngano, mbolea za kemikali na bidhaa nyinginezo, na suala hili limesababisha matatizo ya ziada kwa nchi za Afrika.