Jun 11, 2016 07:35 UTC
  • Burundi: Hatutaki mazungumzo ya amani na upinzani

Licha ya juhudi za kimataifa na za kieneo za kutaka kutatuliwa mgogoro wa Burundi, lakini serikali ya nchi hiyo imesema haiko tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani.

Philippe Nzobonariba, msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza amesema serikali ya nchi hiyo haiwezi kuketi meza moja na wapinzani na makundi ya wabeba silaha yanaonuia kuipindua serikali na kushadishisha ghasia nchini humo. Amesema serikali iko tayari kufanya mazungumzo na wananchi tu ambao wanakaribisha mchakato wa kurejesha utangamano na amani nchini humo. Mazungumzo ya kuukwamua mzozo wa kisiasa nchini Burundi huko mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania, yalifanyika mwezi jana wa Mei bila kuhudhuriwa na muungano mkuu wa upinzani dhidi ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania ambaye pia ni mpatanishi wa mgogoro wa Burundi ameahidi kuzungumza na pande zote hasimu nchini Burundi katika duru ijayo ya mazungumzo, ikiwa ni katika jitihada za kuutatua mgogoro wa nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika.

Kuendelea kusalia madarakani rais huyo na ambako kunatajwa na wapinzani kuwa ni kinyume na katiba na maelewano ya mjini Arusha Tanzania, ndio sababu ya kuibuka hali ya mchafukoge ya zaidi ya mwaka mmoja sasa nchini humo.

Tags