Maandamano ya kupinga siasa za Marekani nchini Ethiopia
(last modified Tue, 25 Oct 2022 09:57:31 GMT )
Oct 25, 2022 09:57 UTC
  • Maandamano ya kupinga siasa za Marekani nchini Ethiopia

Sambamba na kushtadi mapigano nchini Ethiopia na kuvunjwa makubalianao ya usitishaji vita ya miezi mitano na kuwaka tena moto wa vita katika nchi hiyo, maelfu ya Waethiopia walifanya maandamano ya nchi nzima siku ya Jumamosi kulaani uingiliaji wa madola ya kigeni, hasa Marekani, katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Katika mji mkuu Addis Ababa, waandamanaji walibeba mabango yaliyosomeka "Tishio kwa Ethiopia ni tishio kwa ulimwengu" na "heshimu uhuru wa kujitawala Ethiopia." Mabango mengine yalikuwa na maneno ya kuishutumu Marekani kwa kutoheshimu uhuru wa Ethiopia.

Akizungumza mbele ya umati mkubwa, Jantrar Abay, naibu meya wa jiji la Addis Ababa alisema, "Nchi za kigeni zinapaswa kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Ethiopia na zinapaswa kuacha kuunga mkono vikosi vya waasi, haswa kundi la Tigray People's Liberation Front (TPLF) na washirika wake,".

"Utawala wa Ethiopia lazima uheshimiwe, Waethiopia wataendelea kusimama kwa umoja ili kulinda uhuru wa nchi yao", aliongeza.

Maandamano kama hayo yalifanyika pia katika miji mingine mikubwa ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Wapiganaji wa Tigray

 

Tangu mwezi Novemba mwaka 2020 jimbo la Tigray limekumbwa na mivutano ya kisiasa kati ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na viongozi wa eneo hilo ambao wakati fulani waliwahi kuongoza serikali ya Ethiopia. Serikali ya Ethiopia ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed inaituhumu TPLF kwa kujaribu kurejesha utawala wake katika nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika. TPLF iliongoza muungano tawala Ethiopia kwa karibu miaka 30 kabla ya kuondolewa madarakani mwaka 2018 wakati Abiy Ahmed alipoingia madarakani. TPLF inamtuhumu Abiy Ahmed kwa kujiongezea mamlaka na kuwakandamiza Watigray. Ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa znaonyesha kuwa, kwa akali raia 100 wameuawa katika majuma ya hivi karibuni huku wananchi 500,000 wakilazimika kuwa wakimbizi.

Eneo la Pembe ya Afrika ambalo linajumuisha mataifa ya Eritrea, Djibouti, Somalia ana Ethiopia limekuwa likizingatiwa sana na madola makubwa ya kieneo na kimataifa kutokana na kuweko kwake katika eneo muhimu kijiopolitiki na kistratejia.

Eneo hilo ni kiunganishi baina ya Afrika la Peninsula ya Kiarabu na Bahari ya Hindi. Katika upande mwingine, Ghuba ya Aden na Lango Bahari la Bab al-Mandab ni njia kuu ya usafiri na uchukuzi wa matanki ya mafuta kutoka mataifa ya Ghuba ya Uajemi kuelekea katika ulimwengu wa Magharibi. Sifa maalumu liliyonalo eneo hili limelifanya kuwa uwanja wa ushindani wa kieneo na kimataifa kwa ajili ya kupenya na kuwa na ushawishi kwa nchi za eneo. Hivi sasa eneo la Pembe ya Afrika linahesabiwa kuwa, moja ya maeneo ya kistratejia kwa ajili ya ushindani baina ya madola ajinabi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana katika vita baina ya jeshi la Ethiopia na wapiganaji wa Tigray kunashuhudiwa nyayo za kisiasa za Washington.

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia

 

Viongozi wa Marekani ambao tangu awali walikuwa wakipinga Abiy Ahmed kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, hivi sasa wanaituhuhumu serikali yake kwamba, inakiuka haki za binadamu na wamo mbioni kuwa na uwepo na ushawishi zaidi katika eneo hilo. Marekani inafanya juhudi za kuwa na uwepo zaidi katika eneo la Pembe ya Afrika ili iweze kushindana vizuri na mataifa kama Russia na China ambayo yana uwepo amilifu katika miaka ya hivi karibuni barani Afrika hususan katika eneo la Pembe ya Afrika. Misimamo ya viongozi wa Marekani inayotangazwa mara kwa mara kuhusiana nna vita vya sasa vya Tigray imewafanya viongozi wa Addis Ababa kuwatuhumu mara chungu nzima viongozi wa Washington kwamba, wanaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiafrika.

Ni hivi majuzi tu ambapo Taye Dendea Aredo, Waziri Mashauri katika serikali ya Ethiopia alisema kuwa, utendaji wa ubalozi wa Marekani nchini Ethiopa ni wa kigaidi na wautumiaji mabavu na kwamba, ubalozi huo haupaswi kuweko katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiafrika.