Walimu waliombadilishia namba ya mtihani mwanafunzi wa Darasa la 7 Tanzania wafukuzwa kazi
(last modified Wed, 26 Oct 2022 02:33:12 GMT )
Oct 26, 2022 02:33 UTC
  • Walimu waliombadilishia namba ya mtihani mwanafunzi wa Darasa la 7 Tanzania wafukuzwa kazi

Serikali ya Tanzania imeifungia Shule ya Awali na Msingi ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha Mitihani pamoja na kuwafuta kazi wasimamizi wa mtihani ambao ni walimu kutokana na udanganyifu uliofanyika katika Mtihani wa Darsa la Saba uliofanyika tarehe 5 na 6 za mwezi huu wa Oktoba.

Akitangaza uamuzi huo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema uchunguzi uliofanywa na kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani na ule wa wataalamu wa miandiko "forensic" uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini ufanano wa miandiko kwa watahiniwa saba wa shule hiyo.

Uchunguzi huo ulifanywa baada ya kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Ibtisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba, alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) uliofanyika tarehe 5 na 6 za mwezi huu.

Profesa Mkenda ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa hiyo Serikali kupitia Baraza la Mitihani ilielekeza Kamati ya Uendeshaji Mitihani ya Mkoa wa Pwani kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya mtahiniwa na kuwasilisha taarifa Baraza la Mitihani.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania Profesa Adolf Mkenda

"Uchunguzi uliofanyika pia umebaini kuwa mwanafunzi huyo pamoja na wengine sita walibadilishiwa namba ya mtihani katika mtihani wa taifa wa darasa la saba", amefafanua waziri huyo.

Profea Mkenda amesisitiza kuwa kulikuwa na uzembe uliofanyika, hivyo pamoja na kuifungia shule, watumishi wa Serikali ambao walikuwa wasimamizi wa kituo hicho watachukuliwa hatua za kinidhamu ambazo si nyingine bali ni kufutwa kazi.

Aidha kufuatia changamoto hiyo, Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefanya marekebisho ya namba za Mitihani za watahiniwa husika ili kila mtahiniwa aweze kupata matokeo yake halali. 

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu Tanzania amempongeza mwanafunzi Ibtisam kwa ujasiri wa kutoa taarifa; naye mzazi wa mwanafunzi huyo Suleiman Said ameishukuru Serikali kwa kufanyia kazi changamoto hiyo aliyopata mtoto wake na pia vyombo vya habari kwa kuisambaza mpaka ikawafikia walengwa na kuifanyia kazi.../