UN yalaani matamshi ya chuki za kikabila ya Rais wa Gambia
(last modified Sat, 11 Jun 2016 15:29:09 GMT )
Jun 11, 2016 15:29 UTC
  • UN yalaani matamshi ya chuki za kikabila ya Rais wa Gambia

Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Uzuiaji Mauaji ya Kimbari amelaani hotuba ya kichochezi ya Rais Yahya Jammeh wa Gambia ya kutishia kuliangamiza kabila la Mandinka nchini humo.

Adama Dieng, amevieleza vyombo vya habari kuwa siku ya tarehe 3 Juni, wakati Rais Jammeh alipokuwa akihutubia mkutano wa kisiasa katika mji wa Tallinding aliwaita watu wa kabila la Mandinka "maadui na maajinabi" na kutishia kuwaua mmoja baada ya mmoja na kuwaweka mahala ambapo "hata nzi hawezi kuwaona".

Mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa ameshtushwa sana na shutuma hizo za hadharani, kauli zisizo na kiutu na vitisho vya Rais Jammeh dhidi ya watu wa kabila la Mandinka.

Dieng amefafanua kuwa kauli za aina hiyo zinazotolewa na kiongozi wa taifa hazina nadhari na ni hatari sana kwa sababu zinaweza kusababisha mpasuko na mgawanyiko baina ya watu, kueneza shaka na kuchochea machafuko dhidi ya jamii fulani kwa sababu ya asili na utambulisho wao tu.

Mbali na kuashiria matukio ya mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda na Bosnia Herzegovina, Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Uzuiaji Mauaji ya Kimbari amekumbusha kuwa mnamo mwaka 2005 viongozi wote wa mataifa ya dunia waliahidi kutekeleza jukumu la kulinda watu wao na mauaji ya kimbari, jinai za kivita, uangamizaji wa kizazi, jinai dhidi ya binadamu na wao wenyewe kujiepusha na kauli za kichochezi.../