Maelfu ya watu washiriki maandamano dhidi ya Rwanda mjini Goma Kongo DR
(last modified Tue, 01 Nov 2022 07:07:46 GMT )
Nov 01, 2022 07:07 UTC
  • Maelfu ya watu washiriki maandamano dhidi ya Rwanda mjini Goma Kongo DR

Maelfu ya watu wameandamana katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dhidi Rwanda inayodaiwa kuwaunga mkono waasi wa M23, huku uhusiano baina ya nchi hizo mbili ukizidi kuharibika baada ya Kinshasa kumuita nyumbani kaimu balozi wake wa muda aliyeko Kigali.

Maandamano hayo ya jana Jumatatu yamefanyika huku waasi wa M23 wakizidi kujizatiti katika maeneo ya mashambani wanayoyadhibiti.

Mambo Kawaya aliyewakilisha asasi ya kiraia katika maandamano hayo amesema, “tunalaani unafiki wa jamii ya kimataifa kuhusiana na uvamizi wa Rwanda".

Kundi la waasi wa M23 ambalo akthari ya wapiganaji wake ni wa kabila la Tutsi lilianzisha tena mapigano mwishoni mwa 2021 baada ya kubakia kimya kwa miaka kadhaa, likiishutumu serikali ya Kongo DR kwa kutoheshimu makubaliano ya kuwajumuisha wapiganaji wa kundi hilo katika jeshi la nchi hiyo.

Rais Paul Kagame wa Rwanda (kulia) na Rais Felix Tshisekedi wa DRC

Kuibuka tena kwa M23 kumevuruga uhusiano wa kikanda katika eneo la Afrika ya Kati, huku DRC ikimshutumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi hilo la waasi.

Siku ya Jumapili, serikali ya DRC ilimwamuru balozi wa Rwanda mjini Kinshahsa, Vincent Karega, kuondoka nchini ndani ya saa 48. Rwanda ilisema imeupokea uamuzi huo "kwa masikitiko".

Licha ya Rwanda kukanusha rasmi tuhuma za kuliunga mkono kundi la waasi wa M23, ripoti ambayo haijachapishwa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mnamo mwezi Agosti iliashiria kuwa Kigali imekuwa ikilisaidia kijeshi na kuliunga mkono kundi hilo.

Wakati huohuo Rais Paul Kagame wa Rwanda alitangaza jana kuwa amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu namna ya kuondoa hali ya mvutano iliyopo kati ya nchi yake na DRC…/

 

 

 

 

 

 

Tags