Wanajeshi kadhaa DRC wakamatwa mkoani Ituri
Wanajeshi kadhaa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) wametiwa mbaroni katika mkoa wa Ituri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Radio Okapi , Brigedia Jenerali Muhindo Akili Mundos Kamanda wa Kikosi cha 31 cha jeshi la nchi hiyo katika eneo la Mambasa yapata kilomita 165 magharibi mwa Bunia, mji mkuu wa Ituri amesema, "askari wawili katika Kikosi cha 31 cha Jeshi la DRC wamekamatwa."
Mwendesha mashtaka wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema wanajeshi hao wamekamatwa baada ya kubainika kuwa wametekeleza vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya raia wawili.
Brigedia Jenerali Muhindo amesema raia hao wawili waliandika barua ya malalamiko dhidi ya wanajeshi hao na kwa msingi huo wamechukuliwa hatua.
Hayo yanajiri wakati amabo, hivi karibuni ripoti ya siri ya Baraza la Usalama la Umoja wa Matafa imefichua kuwa, Brigedia Jenerali Muhindo alifadhili na kulipa silaha kundi la waasi wa Uganda la ADF kuua raia wa nchi hiyo.
Ripoti hiyo ilisema alilisaidia kundi hilo la waasi wa Uganda kuua raia wa Kongo DR, aliposimamia operesheni iliyopewa jina la Sukola iliyolenga kuzima harakati za waasi hao wa Uganda nchini humo kati ya Agosti mwaka 2014 na Juni mwaka 2015.