Jeshi la Somalia lawaangamiza magaidi 100 wa al Shabab
Serikali ya Somalia imetangaza kuwa imewaangamiza magaidi wa kundi la al Shabab wapatao 100 wakiwemo viongozi 10 wa kundi hilo la kigaidi katika oparesheni iliyofanywa na jeshi kusini mwa nchi.
Abdilrahman Yusuf al Adala, Naibu Waziri wa Habari wa Somalia, alisema jana katika mkutano na waandishi wa habari kuwa jeshi la nchi hiyo limewauwa magaidi 100 wa al Shabab katika oparesheni iliyofanyika katika kitongoji kimoja kinachopatikana baina ya maeneo ya Shabelle ya Kati na Hiran, mbali kuangamiza pia silaha na zana mbalimbali za magaidi hao.
Abdilrahman Yusuf ameongeza kuwa jeshi la Somalia limewafurusha magaidi wa al Shabab katika kitongoji hicho na sasa kinadhibitiwa na jeshi. Viongozi wa Somalia Jumatano iliyopita pia walitangaza kuuliwa magaidi 49 wa kundi hilo la kigaidi katika oparsheni iliyofanywa katika eneo la Shabelle ya Chini nchini humo.
Kabla ya oparesheni hizi, jeshi la Somalia liliwauwa magaidi 21 wa al Shabab katika eneo hilo la Shabelle ya Chini.
Al Shabab ni kundi la kigaidi linalobeba silaha lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida ambalo limehusika katika hujuma na mashambulizi mengi ya kigaidi yaliyouwa mamia ya watu katika nchi mbalimbali barani Afrika.