Wasudan wataka UN iache kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao
Maelfu ya wananchi wa Sudan wamefanya maandamano ya kupinga makubaliano ya amani yanayotazamiwa kusainiwa kesho Jumatatu kwa shabaha ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Maandamano ya jana Jumamosi ni sehemu ya malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Sudan tangu baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa Oktoba 25 mwaka jana, wakitaka nchi ajinabi na taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa ziache kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao.
Waandamanaji walikusanyika nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Khartoum, ambapo walisikika wakipiga nara wakisema "Musiingilie masuala ya Wasudan."
Ahmed Omar, mmoja wa waandamanaji hao amenukuliwa na vyombo vya habari mjini Khartoum akisema kuwa, "Hatuungi mkono mapatano haya."
Wananchi wengine wa Sudan walioshiriki kwenye maandamano ya jana walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kutaka Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Volker Perthes aondoke nchi humo mara moja.
Msudan mwingine aliyeshiriki kwenye maandamano ya jana, kwa jina Mohamed Hasabo amesema akthari ya wananchi wa Sudan hawaungi mkono mchakato huo wa amani unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa, kwani wanahisi si jumuishi.
Makundi ya kiraia kama vile FCC kwa upande mmoja na utawala wa kijeshi unaongoza hivi sasa nchini Sudan kwa upande wa pili zinatazamiwa kusaini makubaliano ya kuhitimisha mzozo wa kisiasa nchini humo kesho Jumatatu.
Hata hivyo mapatano hayo yamepingwa na kukosolewa na Chama cha Wanataaluma wa Sudan (SPA), Chama cha Kikomunisti na makundi mengine madogo ya kisiasa ya nchi hiyo.