DRC: Kwa akali watu 120 wameaga dunia katika janga la mafuriko Kinshasa
(last modified Wed, 14 Dec 2022 03:32:55 GMT )
Dec 14, 2022 03:32 UTC
  • DRC: Kwa akali watu 120 wameaga dunia katika janga la mafuriko Kinshasa

Kwa akali watu 120 wamefariki dunia huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia janga la mafuriko makubwa yaliyoukumba mji huo hapo jana.

Ripoti kutoka nchini humo zinasema kuwa, mvua kubwa imesababisha mafuriko mabaya sana ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Idadi hiyo inaelezwa huenda ikaongezeka wakati serikali ikiendelea na juhudi za uokoaji huku maelfu wakiripotiwa kubakia bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.

Barabara kuu katika mji huo wenye wakaazi milioni 15 zilifunikwa na maji na kusababisha adha kubwa kutokana na kutopitika kwa urahisi. Picha ambazo zinasambazwa mitandaoni zimeonesha maporomoko ya udongo katika wilaya ya Mont-Ngafula na kusababisa mpasuko kwenye barabara muhimu inayounganisha mji mkuu Kinshasa na bandari ya Matadi.Nyumba nyingi ambazo ni mabanda zimejengwa katika maeneo yenye hatari ya kukumbwa na mafuriko, na aghalabu wakaazi huathirika pakubwa.

Maeneio mengi ya Kinshasa yamefunikwa na maji baada ya kutokea mafuriko makubwa

 

Jean-Michel Sama Lukonde, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, timu za uokozi zinaendelea kuwatafuta watu wengine ambao wametoweka na wanaosadikiwa kusombwa na mafuriko hayo.

Mafuriko yalifurika pia barabara katika wilaya ya Gombe ambako kunapatikana soku kuu, wizara za serikali na afisi za balozi.

Blanchard Mvubu, anayeishi Mont-Ngafula, amenukuliwa na duru za habari katika eneo la tukio akisema kuwa, "hatujawahi kuona mafuriko hapa kwa kiwango hiki," "Nilikuwa nimelala, na nilihisi maji ndani ya nyumba ... ni janga. Tumepoteza mali zetu zote ndani ya nyumba, hakuna kitu kinachoweza kuokolewa."

Tags