Waziri Mkuu wa Libya akiri kuhusika katika kuhamishwa mshukiwa wa Lockerbie
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i91784
Waziri Mkuu wa Libya, Abdulhamid al-Dbaiba amekiri kuwa serikali yake imehusika katika kumhamishia wiki iliyopita nchini Marekani Abu Agila Mohammad Masud Kheir al-Marimi mshukiwa katika kesi ya mlipuko wa Lockerbie.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 17, 2022 03:14 UTC
  • Waziri Mkuu wa Libya akiri kuhusika katika kuhamishwa mshukiwa wa Lockerbie

Waziri Mkuu wa Libya, Abdulhamid al-Dbaiba amekiri kuwa serikali yake imehusika katika kumhamishia wiki iliyopita nchini Marekani Abu Agila Mohammad Masud Kheir al-Marimi mshukiwa katika kesi ya mlipuko wa Lockerbie.

Akiwahutubia wananchi wa Libya, Al-Dbaiba ameeleza kuwa, Polisi ya Kimataifa (Interpol) ilitoa waranti wa kumtia nguvuni mshukiwa huyo na kwamba ilikuwa muhimu kwa watu wa Libya kushirikiana katika kadhia hiyo kwa ajili ya maslahi na utulivu wa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa, kuhamishiwa Marekani Abu Agila Muhammad kumefanyika kisheria na serikali yake ilitoa tu ushirikiano kwa mahakama ya kimataifa ili kuwahamisha raia wa nchi hiyo wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali. 

Mshukiwa katika kesi ya Lockerbie, Abu Agila Muhammad 

Katika hutuba yake kwa wananchi, Waziri Mkuu wa Libya hata hivyo hakutoa ushahidi wowote wenye mashiko wa kumtaja Masud kuwa ndiye aliyetengeza bomu lililotumika kulipua ndege ya Pan American iliyouwa watu 207 lakini alisema kwamba, nchi yake ilipaswa "kufuta alama ya ugaidi kwenye paji la uso la watu wa Libya".

Abdulhamid al-Dbaiba amebainisha hayo siku mbili baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa nchi hiyo Siddiq al Sour kutangaza kuwa uchunguzi utafanywa kuhusu mazingira yaliyopelekea kutiwa nguvuni Masud na kuhamishiwa Marekani baada ya familia ya mshukiwa huyo kuwasilisha malalamiko yake.