Ushiriki mdogo wa wananchi wa Tunisia katika uchaguzi wa Bunge
Karibu akthari ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura nchini Tunisia walisusia uchaguzi wa Bunge uliofanyika Jumamosi ya juzi tarehe 17 Disemba.
Tume Huru ya Uchaguzi ya Tunisia ilitangaza baada ya kufungwa vituo vya kupigia kuura siku ya Jumamosi kwamba, karibu asilimia 9 tu ya wananchi wa nchi hiyo ndio walioshiriki zoezi la uchaguzi wa Bunge nchini humo. Hii ni katika hali ambayo asilimia 40 ya wananchi wa Tunisia waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki katka uchaguzi uliopita wa Bunge wa mwaka 2019.
Ushiriki mdogo katika uchaguzi wa Bunge nchini Tunisia umeshuhudiwa baada ya kutolewa miito ya kususia uchaguzi huo kiasi kwamba, hakuna hata mtu mmoja katika kila watu kumi waliotimiza masharti ya kupiga kura ambaye ameshiriki katika zoezi hilo. Mahudhurio madogo ya wananchi wa Tunisia katika uchaguzi wa Bunge wa mara hii ni jambo ambalo lilitarajiwa. Vyama 13 vya upinzani vilitoa mwito wa kususiwa uchaguzi huo vikimtuhumu Rais Kais Saied wa nchi hiyo kwamba, amedhoofisha na kukandamiza demokrasia. Mrengo wa upinzani nchini Tunisia umeutaja uchaguzi wa juzi wa Bunge nchini Tunisia kuwa ni "pigo kubwa" na umemtaka Rais Kais Saied ajiuzulu.
Nejib Chebbi, kiongozi wa Muungano wa Uokovu amesema, matokeo ya awali yanaonesha kuwa, licha ya wananchi milioni 9.3 kutimiza masharti ya kushiriki katika uchaguzi huo ili kuwachagua wabunge 161 kati ya wagombea 1058, lakini ni asilimia 9 tu waliojitokeza kushiriki zoezi hilo.
Amesema, "Kilichofanyika siku yas Jumamosi ni zilzala. Tokea sasa, hatumtambui Saied kama rais halali (wa Tunisia) na tunamtaka ajiuzulu mara moja kufuatia mtikisiko huo."
Vyama vya upinzani nchini Tunisia vinasema, Rais Kais Saied amepoteza uhalali wa kuendelea kuwa kiongozi wa nchi hiyo, baada ya Watunisia wengi kususia uchaguzi huo.
Hata hivyo serikali ya Tunisia inajipapatua na kujaribu kuhalalisha kushindwa huku kukubwa. Farouq Bouasker, Mkuu wa Kamisheni Huru ya Uchaguzi ya Tunisia amekiri kuweko ushiriki mdogo wa wananchi katika uchaguzi wa Bunge wa Tunisia na kudai kwamba, kinyume na chaguzi zilizotangulia, misaada kutoka nje kwa ajili ya kuendeshea zoezi la uchaguzi ilikuwa kidogo. Wakati huo huo, Bouasker amedai kuwa, uchaguzi huo ulikuwa salama nma bila ya kura kununuliwa.
Mnamo Julai 25, 2021, Rais Kais Saeid, alipitisha maamuzi na kuchukua hatua kadhaa zisizo za kawaida ikiwemo kutangaza kufuta mamlaka ya Bunge, kuondolewa kwa kinga ya Wabunge, kumfuta kazi Waziri Mkuu na kuvunja tume ya usimamizi wa katiba, hatua ambazo zilizusha mtafaruku na mkwamo wa kisiasa nchini Tunisia, ambao uliambatana na wimbi la maandamano ya vyama na mirengo ya kisiasa, kikiwemo chama cha Kiislamu cha al-Nahdha.
Lakini mbali na hatua hizo, Julai 25, 2022, Kais Saeid aliitisha kura ya maoni ya katiba mpya ambayo ilipitishwa licha ya kupigiwa kura na Watunisia wachache, ambapo kiwango cha ushiriki katika kura hiyo ya maoni kilitajwa kuwa ni asilimia 27.5. Ushiriki huo wenyewe ulikuwa ni ishara ya wazi ya wananchi wa nchi hiyo ya kulalamikia maamuzi ya Rais Kais Saied.
Wapinzani wanachukulia hatua za Rais wa Tunisia kuwa ni mapinduzi dhidi ya katiba iliyoidhinishwa mwaka 2014 na mabadiliko ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011 yaliyohitimisha utawala wa kidikteta wa Zine El Abidine Ben Ali, lakini Saied mwenyewe anasisitiza kuwa, hatua zake zimelenga kuiokoa Tunisia na msambaratiko wa kiuchumi na kijamii. Katika hatua iliyofuata, Rais wa Tunisia alitangaza kufanya mabadiliko katika sheria za uchaguzi ambapo alidai kuwa, lengo la mabadiliko hayo ni kuzuia ukiukaji wa sheria na maagizo ya kuwachagua Wabunge fulani na vilevile kuzuia kuenea fedha za ufisadi. Miongoni mwa yaliyomo katika sheria mpya za uchaguzi ni kupunguzwa idadi ya viti vya Bunge kutoka 217 na kuwa 161.
Pamoja na hayo yote, ushiriki mdogo wa wananchi wa Tunisia katika uchaguzi wa Bunge wa mara hii ni ishara ya wazi kwamba, wananchi wa nchi hiyo hawana imani tena na Rais Kais Saied, kaulimbiu na hata ahadi zake. Baada ya kuingia madarakani Rais huyo alidai kwamba, mageuzi yake yatalenga kupambana na ufisadi, mkwamo wa kisiasa na mdodoro wa kiuchumi. Awali hatua zake zilipokelewa vizuri na baadhi ya wananchi. Hata hivyo kuendelea hatua na juhudi zake za kuhodhi madaraka, kuzisambaratisha na kuzibinya asasi za kisheria na kutotekeleza ahadi zake ni mambo yaliyopelekea kupungua kupendwa kwake na hata uungaji mkono wa wananchi kwa kiongozi huyo.
Hali ya kukata tamaa iliyoibuka baina ya wananchi wa Tunisia kuhusiana na hali ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo ni mambo yaliyoifanya idadi kubwa ya vijana kukimbilia nje ya nchi kwa lengo la kwenda kutafuta kazi na maisha bora. Rais Kais licha ya kutoa nara na kaulimbiu, lakini hadi sasa hajaja na mpango kabambe wa kuboresha hali ya uchumi na kiwango kikubwa cha ukosefu wa jira.
Maisha ya wananchi wa Tunisia yamezidi kuwa magumu zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Ni kwa muda sasa Tunisia imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa kiuchumi ambapo janga la corona na vita vya Ukraine vimepelekea hali hiyo kuwa mbaya zaidi. Tunisia iliyoko kaskazini mwa Afrika inategemea mno uingizaji wa bidhaa kama za mafuta na nafaka kutoka nje ya nchi.