Dec 24, 2022 06:01 UTC
  • Waasi wa M23 huko DRC kuondoka mji wa kistratajia wa Kibumba

Kundi la waasi wa M23 limeahidi kuondoka katika mji wa kistratajia wa Kibumba karibu na jiji la Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, kundi la M23 limetangaza utayarifu wake wa kuondoka katika mji wa Kibumba, yapata kilomita 20 kutoka mji wa kibiashara wa Goma wenye wakazi milioni moja.   

M23 imesema itaukabidhi mji huo kwa vikosi vya kieneo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kama ishara ya irada njema inayoenda sambamba na mazungumzo ya amani ya hivi karibuni ya Luanda, mji mkuu wa Angola. Waasi hao wameitaka serikali ya Kinshasa 'kukumbatia fursa hii kwa mikono miwili.'

Mapema mwezi huu, wanamgambo hao wa M23 walikubali kuondoka pia katika eneo jingine lililokuwa chini ya udhibiti wao, ikiwa ni pamoja na mpaka wa Bunagana na vitongoji vya Kitigoma mashariki mwa DRC.

Mpango wa hivi majuzi wa amani unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki uliamuru kusitishwa kwa mapigano na kuondoka waasi wa M23 kutoka maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Hata hivyo waasi wa M23 wamekaidi wito wa kusitisha vita na wangali wanakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya mashariki mwa DRC.

Serikali ya DRC inaituhumu nchi jirani ya Rwanda kuwa ndiyo inayowaunga mkono waasi hao wa M23. Hata hivyo Rwanda mara kadhaa imekanusha vikali tuhuma hizo.

Tags