Kenya kupeleka vikosi maalumu pwani na kaskazini kukabiliana na ukosefu wa usalama
(last modified Thu, 21 Sep 2023 02:35:03 GMT )
Sep 21, 2023 02:35 UTC
  • Kenya kupeleka vikosi maalumu pwani na kaskazini kukabiliana na ukosefu wa usalama

Serikali ya Kenya inapanga kupeleka vikosi maalumu katika maeneo ya kaskazini na pwani ili kukabiliana na tishio la ugaidi kufuatia ongezeko la mashambulizi ya kigaidi katika maeneo hayo.

Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa wa Kenya, Kithure Kindiki, alitangaza uamuzi huo jana Jumatano saa chache baada ya mtu mmoja kuuawa, na nyumba kadhaa kuteketezwa na kuwa majivu katika hujuma ya watu wanaoshukiwa kuwa magaidi wa al Shabaab katika kijiji kimoja Kaunti ya Lamu.

Eneo hilo la pwani limekuwa likilengwa na mashambulizi ya magaidi wanaoaminika kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la al Shabaab lenye makao yake nchini Somalia.

Kindiki alisema kuwa: "Ili kukabiliana vilivyo na tishio la ugaidi na itikadi kali za kikatili, serikali inatuma maeneo ya Kaskazini mwa Kenya na Pwani, zikiwemo Kaunti za Tana River na Lamu, vikosi maalumu ili kuwasaka na kuwazuia wahalifu wenye silaha ambao wanawatisha raia wasio na hatia."

Wiki iliyopita, idadi isiyojulikana ya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya waliuawa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupita juu ya bomu iliyotegwa barabarani huko Lamu.

Jeshi limetuma maafisa zaidi kukabiliana na tishio la al-Shabaab katika eneo hilo ambalo linakaribia mpaka wa Kenya na Somalia.

Siku ya Jumatatu, wanajeshi wengine kadhaa waliuawa katika ajali ya helikopta.

Operesheni ya usalama ya mashirika kadhaa ya usalama pia inaendelea katika eneo la kaskazini mwa Kenya ambalo linatatizwa na hujuma za kigaidi za mara kwa mara.