Shirika la ndege la Ethiopia kuanza tena safari zake huko Tigray
Shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines) limetangaza kuwa linaanza tena safari zake katika eneo la Tigray lililoathiriwa na machafuko huko kaskazini mwa Ethiopia sambambana eneo hilo kuunganishwa katika gridi ya taifa ya umeme na kurejeshewa huduma za simu na nyinginezo.
Shirika la ndege la Ethiopia kesho Jumatano litaanza tena safari kuelekea Tigray. Safari hiyo ni ya kwanza ya kibiashara kufanyika katika eneo hilo katika kipindi cha miezi 18 kufuatia vita vilivyokuwa vikiendelea huko Tigray.
Shirika la Ethiopian Airlines limetoa taarifa hii siku moja baada ya ujumbe wa maafisa wa serikali ya nchi hiyo na wakurugenzi wa mashirika ya umma kutembelea mji wa Mekelle kujadili namna ya kutekeleza mapatano ya amani yaliyofikiwa mwezi uliopita kati ya serikali ya Addis Ababa na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF). Mapatano hayo yalifikiwa ili kuhitimisha mzozo huko Tigray.
Mapatano hayo ya amani kati ya Addis Ababa na harakati ya TPLF ambayo yamejumuisha ahadi za kurejesha huduma mbalimbali huko Tigray yamehitimisha miaka miwili ya mapigano kati ya serikali kuu ya Ethiopia na waitifaki wake dhidi ya wapiganaji wa Tigray; mapigano ambayo hadi sasa yameuwa maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Mesfin Tasew Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia amesema kuwa, kuanza tena kwa safari za ndege kuelekea Tigray kutaziwezesha familia mbalimbali kuungana na jamaa zao, kurahisisha biashara, kuchochea utalii na kufungua fursa zaidi ambazo zitaisaidia jamii. Mesfin ni sehemu ya ujumbe wa serikali ya Ethiopia ambao jana ulielekea huko Mekelle kujadili namna ya kutekeleza mapatano ya amani.
Huku haya yakiripotiwa, wakala wa usafirishaji katika mji mkuu Addis Ababa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, tiketi zote za safari ya kwanza ya ndege kuelekea Mekelle zimenunuliwa ndani ya saa chache baada ya kutolewa tangazo hilo.