Kongamano la kwanza la UN kuhusu Albino Afrika kufanyika Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9268-kongamano_la_kwanza_la_un_kuhusu_albino_afrika_kufanyika_tanzania
Kongamano la kwanza la kikanda linalofadhiliwa na Umoja wa Mataifa la kuzungumzia hatua za kuchukua kwa ajli ya watu walemavu wa ngozi (Albino) linatazamiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu katika mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam kuanzia hapo kesho Ijumaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2016 23:20 UTC
  • Kongamano la kwanza la UN kuhusu Albino Afrika kufanyika Tanzania

Kongamano la kwanza la kikanda linalofadhiliwa na Umoja wa Mataifa la kuzungumzia hatua za kuchukua kwa ajli ya watu walemavu wa ngozi (Albino) linatazamiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu katika mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam kuanzia hapo kesho Ijumaa.

Kongamano hilo litalenga kuratibu hatua maalumu za kukabiliana na hujuma na ubaguzi wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi katika nchi kadhaa za Afrika.

Kongamano hilo litafanyika kwa kaulimbiu ya 'Vitendo Zaidi Kuliko Maneno'.

Watu wa jamii ya Albino katika eneo la Chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika wanakabiliwa na baadhi ya aina mbaya zaidi za ukiukaji wa haki za binadamu. Watu hao wanashambuliwa na kudhuriwa kimwili kwa sababu ya imani potofu kwamba viungo vya miili yao vinaweza kutumiwa kama dawa ya mapenzi na katika vitendo vingine vya uchawi na ushirikina. Waathiriwa wakubwa zaidi wa hujuma hizo za kinyama ni wanawake na watoto.

Maalbino wanakabiliwa pia na ubaguzi na kutengwa na jamaa wa familia hususan mama wenye watoto wenye ulemavu huo wa ngozi.

Ikponwosa Ero, mtaalamu wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Albino amesema, baada ya siku ya kimataifa ya kujenga uelewa kuhusu Albino iliyofanyika Jumatatu ya tarehe 13 mwezi huu, zaidi ya watu 150 kutoka nchi 28 za Kiafrika watakutana mjini Dar se Salaam kuandaa ramani ya njia ya hatua maalumu za kuchukua ili kushughulikia masuala ya haki za binadamu yanayowakabili watu wenye ulemavu wa ngozi.

Karibu nusu ya washiriki wa kongamano hilo wanatoka kwenye asasi za kiraia, asilimia 20 wanatoka kwenye taasisi za serikali, asilimia 10 ni kutoka taasisi za kitaifa za haki za binadamu na washiriki wengine ni wataalamu wa haki za binadamu kutoka ndani na nje ya Umoja wa Afrika pamoja na wanaakademia wa Umoja wa Mataifa.../