Niger yasema wahajiri 34 wameaga dunia wakielekea Ulaya
(last modified Thu, 16 Jun 2016 15:30:51 GMT )
Jun 16, 2016 15:30 UTC
  • Niger yasema wahajiri 34 wameaga dunia wakielekea Ulaya

Serikali ya Niger imesema wahajiri 34 raia wa nchi kadhaa za Afrika wakiwemo watoto wadogo 20 wameaga dunia katika jangwa la nchi hiyo baada ya kutelekezwa na mtu aliyekuwa akiwapeleka barani Ulaya.

Bazoum Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika amesema miili ya wahajiri hao imepatikana katika eneo lenye joto kali la Agadez, kaskazini mwa nchi, baada ya kuachwa na mtu aliyekuwa akiwasafirisha kwenda Ulaya kupitia Jangwa la Sahara, pwani ya Libya na kisha Bahari ya Mediterranean. Amesema mbali na miili 20 ya watoto wadogo, miili 14 ya watu wazima inajumuisha 9 ya wanawake na 5 ya wanaume. Waziri wa Mambo ya Nje wa Niger ameongeza kuwa, yumkini wahamiaji hao walipoteza maisha kati ya Juni 6 na 12 na kwamba miili miwili miongoni mwayo ni ya raia wa nchi jirani ya Nigeria.

Hivi karibuni, Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR lilisema kuwa, yumkini watu 700 wameaga dunia baada ya boti zao kuzama katika Barahari ya Mediterranean na kisha miili yao kupatikana katika pwani ya Libya. Habari ziliarifu kuwa, aghalabu ya wahajiri waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni raia wa nchi za Kiafika kama Somalia, Sudan, Ethiopia na Misri.

Wahajiri karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku wengine 2,000 wakifariki dunia kwa kuzama baharini.

Tags