Tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim yakosa mshindi 2015
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9325-tuzo_ya_kifahari_ya_mo_ibrahim_yakosa_mshindi_2015
Wakfu wa Mo Ibrahim umetangaza kwamba hakukuwa na mshindi wa tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim mwaka jana 2015.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2016 11:01 UTC
  • Tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim yakosa mshindi 2015

Wakfu wa Mo Ibrahim umetangaza kwamba hakukuwa na mshindi wa tuzo ya kifahari ya Mo Ibrahim mwaka jana 2015.

Dakta Salim Ahmed Salim, mwenyekiti wa kamati huru iliyosimamia tuzo hiyo mwaka huu amesema kuwa, tuzo hiyo ambayo hutolewa mahsusi kwa marais wastaafu barani Afrika haikupata mshindi mwaka jana 2015. Dakta Salim ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania amesema hakuna rais mstaafu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita aliyetimiza vigezo vilivyowekwa na kamati yao. Dakta Mo Ibrahim, mwenyekiti wa Wakfu wa Mo Ibrahim na muasisi wa tuzo hiyo amesema: "Bodi inaheshimu maamuzi ya kamati huru ya tuzo hiyo. Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita tangu tuanze kutoa tuzo hii tuliweka viwango vya juu kwa shabaha ya kuimarisha demokrasia na mfumo wa uongozi barani Afrika. Lengo letu ni kuwatunuku viongozi wenye haiba na ustahiki wa kutuzwa." Huku ni kusema kuwa, marais waliostaafu hivi karibuni kama vile Jakaya Kikwete wa Tanzania, Goodluck Jonathan wa Nigeria na Armando Guebuza wa Msumbiji wameambulia patupu katika tuzo hiyo ya kifahari ya mwaka jana, huku Mwai Kibaki wa Kenya akikosa kutuzwa mwaka 2014. Tuzo hiyo ambayo tangu kuasisiwa kwake mwaka 2006 imetunukiwa viongozi wanne pekee, huwalenga marais ambao walichaguliwa kwa misingi ya demokrasia na kuhudumu katika muhula ulioanishwa na katiba pasina kung'ang'amia madaraka wala kuongoza kwa mkono wa chuma. Rais mstaafu wa mwisho kutuzwa tuzo ya Mo Ibrahim ni Hifikepunye Pohamba wa Namibia (2014). Wengine ni Pedro Pires wa Cape Verde (2011), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Joaquim Chissano wa Msumbiji (2007). Mshindi wa tuzo hii hukabidhiwa dola milioni 5 pesa taslimu katika muda wa muongo mmoja hivi na kisha dola laki mbili kila mwaka katika kipindi cha uhai wake.