Watu 74 wauawa na kujeruhiwa katika mapigano yaliyotokea Somalia
Feb 07, 2023 07:11 UTC
Watu wapatao 34 wameuawa katika mapigano ya umwagaji damu yaliyotokea kati ya wanajeshi wa Somalia na wanamgambo katika eneo la Somaliland.
Maafisa wa eneo hilo wamesema, mapigano kati ya vikosi vya usalama vya serikali na wanamgambo kaskazini mwa Somalia yalianza baada ya watu wenye silaha kushambulia kambi ya wanajeshi wa Somalia katika mji wa Laskanud ulioko katika eneo la Somaliland.
Mohammed Farah, mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Laskanud, amesema: "baada ya mapigano kuanza, tuliona maiti na majeruhi wakiingizwa hospitalini. Takriban watu 34 wameuawa katika mapigano hayo na wengine 40 wamejeruhiwa.
Ufyatulianaji risasi huo baina ya wanajeshi wa Somalia na wanamgambo, ambao ulitokea jana asubuhi, umejiri siku moja baada ya maafisa wa eneo hilo, viongozi wa kidini, na maafisa wa kikundi cha jamii nchini Somalia kutangaza kwamba hawawatambui viongozi wa Somaliland.
Kufikia sasa, hakuna upande maelezo yoyote kuhusiana na tukio hilo la jana.
Somaliland ni eneo la kaskazini mwa Somalia ambalo lilijitangazia uhuru mwaka 1991 na kujitenga na ardhi ya nchi hiyo. Hata hivyo, hakuna nchi yoyote hadi sasa ambayo imeutambua uhuru wa eneo hilo.
Somalia ni nchi ambayo kwa miongo mitatu sasa imekuwa ikikabiliwa na matatizo kadhaa kutokana na kuwepo kwa mizozo ya ndani, mashambulizi ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab, kukosekana serikali kuu yenye nguvu, na mgawanyiko kati ya makundi ya kisiasa.../
Tags