Afwerki: Madai kwamba Eritrea imekiuka haki za binadamu Tigray, ni njozi tupu
(last modified Fri, 10 Feb 2023 02:54:49 GMT )
Feb 10, 2023 02:54 UTC
  • Afwerki: Madai kwamba Eritrea imekiuka haki za binadamu Tigray, ni njozi tupu

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki jana Alhamisi aliyataja madai ya kukiukwa haki za binadamu kulikofanywa na wanajeshi wa Eritrea katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia wakati wa vita vya miaka miwili katika eneo hilo kuwa ni njozi tupu.

Rais wa Eritrea ameeleza hayo akiwa ziarani Kenya katika mkutano na waandishi wa habari akijibu swali kuhusu  uwepo wa wanajeshi wa nchi yake huko Ethiopia. Jeshi la Eritrea liliviunga mkono vikosi vya ulinzi vya Ethiopia katika vita kati ya serikali ya Addis Ababa na harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).  

Wapiganaji wa TPLF 

Vita hivyo vimemalizika kwa kusainiwa makubaliano ya amani mwezi Novemba mwaka jana; makubaliano ambayo yalitaka kuondoka vikosi vya nchi ajinabi huko Tigray hata hivyo jina la Eritrea halikuashiriwa rasmi; nchi ambayo serikali yake inaihesabu harakati ya wapiganaji wa TPLF kuwa ni adui wake. 

Wakazi wa eneo la Tigray ambao wanawatuhumu wanajeshi wa Eritrea kwa mauaji, vitendo vya ubakaji na  kupora mali za raia wanasema kuwa Asmara haikuwa sehemu ya makubaliano hayo ya amani na kwamba wanajeshi wa Eritrea bado wapo katika baadhi ya maeneo ya Tigray. 

Alipoulizwa kuhusu kuendelea kuwepo wanajeshi wa Eritrea huko Tigray, Rais wa nchi hiyo Isayas Afwerki amesema kuwa hana nia ya kuingia kadhia hiyo licha kampeni ya upotoshaji inayoendelea kwa lengo la kuvuruga mchakato wa amani huko Ethiopia na kujaribu kuibua mzozo kati ya Eritrea na Ethiopia.