Umoja wa Mataifa watahadharisha juu ya hali ya kiusalama DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9430-umoja_wa_mataifa_watahadharisha_juu_ya_hali_ya_kiusalama_drc
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, yumkini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikatumbukia katika wimbi la ghasia za uchaguzi kama Burundi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2016 03:37 UTC
  • Umoja wa Mataifa watahadharisha juu ya hali ya kiusalama DRC

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, yumkini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikatumbukia katika wimbi la ghasia za uchaguzi kama Burundi.

Kundi la wataalamu waandamizi wa umoja huo limesema kushindwa kufahamika iwapo uchaguzi mkuu nchini Kongo DR utafanyika katika tarehe iliyopangwa yaani mwezi Novemba mwaka huu au la, huenda kukaitumbukiza nchi hiyo katika machafuko. Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na wataalamu hao wa UN imesema kuwa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi ni katika nchi ambazo ziko kwenye ncha ya ghasia na kwamba zitapigwa darubini na umoja huo katika muda wa miezi 6 ijayo. Kadhalika wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wameonya dhidi ya kukandamizwa wananchi na viongozi wa upinzani nchini humo kuelekea uchaguzi mkuu. Wamesema maafisa usalama wa nchi hiyo wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya upinzani, huku wakiashiria maandamano ya hivi karibuni mjini Lubumbashi, ambapo wafuasi wa mgombea wa urais mwenye ushawishi mkubwa Moise Katumbi walitawanywa kwa mabomu ya kutoa machozi. Serikali ya DRC inadai kuwa, ina nyaraka na ushahidi unaoonesha kuwa, Meya huyo wa zamani wa Katanga alihusika katika kusajili mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wa Kimarekani waliostaafu kwa lengo la kutekeleza njama dhidi ya taifa. Itakubukwa kuwa, hivi karibuni Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ilitoa uamuzi kuwa Rais Joseph Kabila anaweza kuendelea kusalia madarakani hata baada ya kumalizika muda wa uongozi wake mwaka huu wa 2016.