Mar 06, 2023 02:37 UTC
  • Wanajeshi 100 wa Burundi wawasili Goma, mashariki mwa DRC

Wanajeshi wapatao 100 wa Burundi wamewasili katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kujiunga na kikosi cha kimataifa kinachosaidia Kinshasa kukabiliana na ongezeko la wanamgambo wenye silaha katika eneo hilo.

Wanajeshi hao wa Burundi wametumwa kama sehemu ya kikosi cha kikanda kilichoundwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujaribu kukomesha uasi wa kundi la M23 na kusambaratisha makundi takriban mia moja yenye silaha ambayo yanaendesha harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilituma wanajeshi mwishoni mwa mwaka jana katika eneo hilo.

Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini yamesababisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao na kuzidisha mivutano ya kikanda, huku serikali ya DRC ikiishutumu Rwanda kwamba, inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo yanakanushwa vikali na serikali ya Kigali ingawa yanaungwa mkono na madola ya Magharibi.

Waasi wa M23 wamehatarisha usalama katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Wanamgambo hao waliibuka tena kutoka katika hali ya utulivu mwishoni mwa 2021, na baadaye kudhibiti maeneo mengi ya Kivu Kaskazini, ikiwa ni pamoja na eneo kubwa la kaskazini mwa jiji la Goma.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo imefanya mikutano kadhaa ya kusuluhisha mzozo huo na kutoa mwito wa kuondolewa waasi wa M23 kutoka maeneo waliyoyateka na kuyakalia kwa mabavu, iliunda kikosi cha kikanda kama sehemu ya jitihada za kudumisha amani na utulivu mashariki mwa DRC. Lakini maelfu ya watu waliandamana mjini Goma mwezi uliopita, wakilituhumu jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutokuwa na msimamo imara mbele ya makundi ya waasi.