Mar 12, 2023 02:56 UTC
  • Kundi la Daesh latangaza kuhusika na jinai nyingine katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika na jinai nyingine ya mwanzoni mwa mwezi huu wa Machi katika kijiji kimoja katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya kundi la kigaidi la Daesh imeeleza kuwa, wanachama wake ndio waliotekeleza shambulio la mwanzoni mwa mwezi huu huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambalo lilipelekea kwa akali watu 35 kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imezidi kuzorota kutokana na harakati za makundi ya waasi katika maeneo hayo.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, limesema limesikitishwa sana na mapigano makali kati ya makundi yasiyo ya wanamgambo yenye silaha na vikosi vya serikali yanayowafanya mamia kwa maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa shirika hilo Matthew Saltmarsh mjini Geniva Uswisi wakati wa mkutano na waandishi wa habari “Mwezi Februari pekee, karibu watu 300,000 walikimbia katika maeneo ya Rutshuru na Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini.”

Ghasia zimeongezeka hususan kuanzia mkoa wa Kitchanga katika eneo la Masisi kuelekea mji muhimu kimkakati wa Sake, huku watu 49,000 wakilazimika kuyahama makazi yao katika wiki ya tarehe 17 Februari.

Serikali ya Kinshasa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kusimamia Amani DRC (MONUSCO) wanakosolewa kwa kushindwa kurejesha amani na usalama katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.