Magaidi wa al-Shabaab wapigana wenyewe kwa wenyewe Somalia
Makundi hasimu ya genge la kigaidi la al-Shabaab la Somalia yameshambuliana katika jimbo lenye mamlaka ya ndani la Puntland.
Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, mapigano hayo yamefanyika katika eneo la Bari mashriki mwa Somalia, baina ya wapiganaji wa al-Shabaab wenye mfungamano na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) na mahasimu wao waitifaki wa mtandao wa al-Qaeda.
Mkuu wa Wilaya ya Qandala, Ahmed Yusuf amethibitisha habari hiyo ya kushambuliana makundi hasimu ya al-Shabaab katika eneo dogo la Balli Dhidin, lililopo baina ya vijiji vya Qandala na Bosaso, yapata kilomita 1500 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.
Wanachama wa al-Shabaab watiifu kwa Sheikh Abdulkadir Mumin walijitenga na kundi mama la al-Shabaab mwaka 2015, na kutangaza utiifu wao kwa Abu Bakr Al-Baghdadi. Mwaka 2019, Marekani ilidai kuwa imemuua kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr al-Baghdadi
Mkuu wa Wilaya ya Qandala amesema hali ya taharuki ingali imetanda katika maeneo hayo ya Puntland, huku wakazi wake wakiishi kwa hofu ya kushambuliwa na magaidi hao.
Puntland inashuhudia mapigano hayo katika hali ambayo, eneo jingine lililotangaza kujitenga na Somalia la Somaliland huko kaskazini mwa nchi limeshuhudia hali ya mchafukoge katika siku za karibuni, kufuatia kuibuka mivutano kati ya mamlaka za utawala na makundi ya koo katika eneo hilo.