Mauritania yakanusha kiuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i95134-mauritania_yakanusha_kiuanzisha_uhusiano_wa_kawaida_na_utawala_wa_kizayuni
Serikali ya Mauritania imekanusha madai ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa inafanya nao mashauriano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 15, 2023 11:06 UTC
  • Mauritania yakanusha kiuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni

Serikali ya Mauritania imekanusha madai ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa inafanya nao mashauriano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Nouakchott hivi karibuni, msemaji wa serikali ya Mauritania, An-Nafi Ould Chrougha, huku akikanusha madai ya vyombo vya habari vya Kizayuni kuhusu kuwepo mashauriano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Tel Aviv na Nouakchott, amesema: Sisi hatuna mawasiliano wala mashauriano yoyote na Israel.

Mauritania ilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel mwaka 1999 wakati wa utawala wa Kanali Muawiya Ould Sidi Ahmad Taya. Hata hivyo, katika kujibu mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mwaka 2009, rais mwingine wa zamani wa nchi hiyo Mohammad Ould Abdulaziz alisimamisha kwa muda uhusiano huo na hatimaye kuukata kabisa mwaka 2010.

Rais Mohamed Ould Cheikh Mohamed Ahmed Ould Ghazouani wa Mauritania

Kukadhibishwa madai ya utawala wa Kizayuni ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Mauritania ni pigo jingine kwa uwepo wa utawala huo wa Kizayuni barani Afrika. Juhudi za utawala huo za kuanzisha uhusiano na Mauritania zinafanyika katika fremu ya mpango mpana wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, unaojulikana kwa jina la Abraham unaolenga kuanzsiha uhusiano kati ya utawala huo wa kibaguzi na nchi za Kiarabu. Pamoja na kuwa kasi ya mpango huo imepungua kufuatia kuondoka madarakani Trump huko Marekani, lakini bado utawala huo unaufuatilia kwa nguvu zake zote ili kuendeleza mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu za Asia Magharibi, Afrika na hata Asia Mashariki.

Pamoja na hayo lakini juhudi hizo zimekabiliwa na upinzani mkali wa kieneo na kimataifa kutokana na siasa na vitendo vya ubaguzi na jinai za kitisha zinazotekelezwa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na vilevile kuendelezwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Beitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Kwa kadiri kwamba hata nchi za Kiarabu kama vile Imarati, ambazo tayari zimetangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo, sasa zimeingiwa na wasiwasi na hivyo kuamua kupunguza kasi ya kuimarisha uhusiano na utawala huo. Kuhusiana na hilo Imarati imefuta makubaliano yake ya silaha na utawala wa Kizayuni na wakati huo huo kuahirisha kwa mara ya tano mfululizo safari ya waziri mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu katika nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi.

Katika bara la Afrika, wimbi kubwa la upinzani dhidi ya Israel limeibuka. Thibitisho la wazi la suala hilo ni kufukuzwa kwa fedheha hivi karibuni ujumbe wa utawala wa Kizayuni katika kikao cha Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, pamoja na azimio la umoja huo la kuwataka wanachama wake wakate uhusiano wao na utawala wa Kizayuni. Azimio hilo linaeleza kuwa nchi wanachama hazipaswi kutambua rasmi mamlaka na hali isiyokuwa ya kisheria inayotekelezwa na utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na maeneo mengine ya Kiarabu, likiwemo la mashariki mwa mji wa Quds, hali inayopelekea maeneo hayo kutambulika kuwa yanakaliwa kikoloni na kwa msingi wa ubaguzi wa rangi.  Pia linazitaka nchi wanachama kukata na utawala huo ghasibu mabadilishano yoyote ya moja kwa moja na yasiyo ya moja kwa moja ya kiutamaduni, kisayansi na kibiashara.

Kuhusiana na suala hilo na kinyume na madai ya utawala haramu wa Israel, Mauritania si tu kwamba haijachukua hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo, bali kimsingi imekanusha kuwepo kwa jambo kama hilo. Tangu mwezi uliopita, vyombo vya habari vya Kizayuni vimekuwa vikizungumzia suala la kuanzishwa uhusiano kati ya utawala wa Kizayuni na Mauritania. Kuhusiana na hilo, gazeti la Kizayuni la Israel Hayom linadai kuwa mazungumzo na mashauriano ya kina yanafanyika na nchi nne ili kuanzisha nazo uhusiano wa kawaida katika fremu ya mpango wa Abraham, na kwamba wizara ya mambo ya nje ya utawala huo inayoongozwa na Eli Cohen inaendeleza juhudi za kuanzisha uhusiano na Mauritania, Somalia, Niger na Indonesia. Gazeti hilo limedai kuwa mashauriano na Mauritania yamepiga hatua kubwa zaidi kuliko nchi nyingine, na kwamba katika kikao chake cha huko nyuma na Analena Baerbock, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Cohen alimtaka rasmi atumie uhusiano wake kuusaidia utawala wa Kizayuni kuanzisha uhusiano wa kawaida na Mauritania na vilevile Niger.

Eli Cohen

Hii ni katika hali ambayo tangu mwaka 2021 wanazuoni na maimamu wa swala ya Ijumaa 200 wa Mauritania wametoa fatwa za kuharamisha kuanzishwa uhusiano na utawala wa Kizayuni. Wametangaza hadharani kwamba ni haramu kuwa na uhusiano wa aina yoyote na utawala huo ghasibu na kwamba hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha uhusiano wa aina hiyo.