Mashambulio ya kigaidi ya Al-Shabaab yaua zaidi ya watu 30 Somalia
Mar 31, 2023 07:14 UTC
Watu zaidi ya 30 wameuawa katika mashambulio yaliyofanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab kusini mwa Somalia.
Kundi la kigaidi la al-Shabaab linadhibiti baadhi ya vijiji na miji kusini mwa Somalia na mara kwa mara hulenga vikosi vya usalama na raia kwa mashambulio ya utegaji mabomu katika mji mkuu Mogadishu na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo.
Katika miezi michache iliyopita, vikosi vya Somalia viliweza kukomboa na kuweka chini ya udhibiti wake makumi ya miji, vitongoji na vijiji vilivyokuwa vikikaliwa na kundi la kigaidi la al-Shabaab.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la habari la IRNA alfajiri ya kuamkia leo, wanajeshi 32 wa Somalia wameuawa katika mashambulizi mawili yaliyofanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab katika maeneo ya Jubaland na Hirshbili, kusini mwa nchi hiyo.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limedai kuwa limeteka kambi kadhaa za jeshi la Somalia baada ya kutekeleza mashambulizi hayo mawili ya kigaidi.
Tangu Julai 2022, vikosi vya serikali vya jeshi la Somalia vimeanza operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab kwa ushirikiano na wanamgambo wanaobeba silaha wa jamii za jadi.
Kwa kuanza kwa operesheni hiyo, Somalia ilitangaza kuwa, mbali na kuyakomboa maeneo kadhaa ya kistratejia yaliyokuwa yakishikiliwa na al-Shabaab imeua pia mamia ya wanamgambo wa kundi hilo la ukufurishaji.
Kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo lilitangaza kuwepo kwake mwanzoni mwa 2004, ni tawi la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, na limeshakiri kuhusika na operesheni nyingi za kigaidi barani Afrika ambazo zimesababisha vifo vya mamia ya watu.../
Tags