Hafla kubwa zaidi ya futari yafanyika Ethiopia
Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Ethiopia limefanya hafla kubwa zaidi ya Iftar katika uwanja wa Al-Thaura mjini Addis Ababa, mji mkuu wa nchi hiyo, wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, kitanga cha Iftar hiyo, ambayo ndiyo kubwa zaidi ya pamoja nchini Ethiopia, kilifunika eneo la takriban la mita za mraba 1,500.
Vyombo vya habari nchini Ethiopia vilmekadiria idadi ya washiriki katika hafla hiyo ya iftar kuwa zaidi ya watu elfu 40, na kwamba watu elfu tatu wamejitolea kuwahudumia Waislamu waliokuwa wamefunga.
Shughuli mbalimbali za kidini na kitamaduni zilifanyika pembezoni mwa hafla hiyo ya iftar.
Akihutubia hafla hiyo, Mkuu wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Ethiopia amewaomba raia wa nchi hiyo kuwasaidia watu wasiojiweza na waliojeruhiwa katika maeneo yaliyoshuhudia majanga ya asili.
Mashirika ya Magharibi yanadai kuwa Waislamu wanaunda thuluthi moja ya wananchi milioni 110 wa Ethiopia.