Guterres: Somalia inahitaji misaada na kuungwa mkono pakubwa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96158-guterres_somalia_inahitaji_misaada_na_kuungwa_mkono_pakubwa_kimataifa
Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyeko ziarani nchini Somalia katika eneo la Pembe ya Afrika leo ametaka kupatiwa misaada na kuungwa mkono pakubwa kimataifa Somalia katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo inakabiliana na janga la kibinadamu lililosababishwa na ukame na ukosefu wa amani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 11, 2023 12:01 UTC
  • Guterres: Somalia inahitaji misaada na kuungwa mkono pakubwa kimataifa

Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyeko ziarani nchini Somalia katika eneo la Pembe ya Afrika leo ametaka kupatiwa misaada na kuungwa mkono pakubwa kimataifa Somalia katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo inakabiliana na janga la kibinadamu lililosababishwa na ukame na ukosefu wa amani nchini humo.

Guterres amesema leo katika mkutano na waandishi wa habari huko Mogadishu akiwa pamoja na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia kuwa: yuko katka ziara ya kuonyesha mshikamamo na nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iliyoko katika hali ya mgogoro; ambako watu milioni tano wanasumbuliwa na  uhaba mkubwa wa chakula. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Niko hapa kupaza sauti kuhusu mahitaji na msaada mkubwa wa kimataifa unaohitajika kwa ajili ya Somalia kwa sababu ya matatizo ya kibinadamu inayopitia nchi hii."

Umoja wa Mataifa umeanzisha mchango wa jumla ya dola bilioni 2.6 za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Somalia ambapo Guterres amesema ni asilimia 15 tu ya maombi ya fedha hizo ndizo zilizopatikana hadi sasa. 

Ukame mkubwa sana ulioiathiri Somalia katika miongo ya karibuni umepelekea aghalabu ya wananchi wa Somalia kukumbwa na njaa huku serikali ya nchi hiyo pia ikiendesha mashambulizi makubwa ya kulitokomeza kundi la wanamgambo wa al Shaabab.

Somalia na ukame mkubwa 

Katibu Mkuu wa UN ambaye yuko katika ziara yake ya kwanza huko Somalia tangu mwezi Machi 2017, amepanga kuitembelea pia kambi ya wakimbizi wa ndani kabla ya kuondoka Somalia kesho Jumatano. 

Katika mkutano huo na waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, naye Rais wa Somalia  Hassan Sheikh Mohamud amesema kuwa ziara ya Guterres nchini humo ni ishara ya kudhihirisha mshikamamo na serikali ya Somalia na mchakato wa demokrasia unaotekelezwa na nchi hiyo.