Kuongezwa nguvu za kijeshi za Umoja wa Ulaya nchini Libya
Umoja wa Ulaya umeamua kuongeza nguvu zake za kijeshi katika opereseheni zake za baharini maarufu kwa jina la Operesheni Sophia, nchini Libya.
Shirika la habari la AFP limetangaza habari hiyo na kusema kuwa, katika kikao chao cha leo Jumatatu mawaziri wa mambo ya nje wa umoja wa Ulaya wamefikia makubaliano ya kuongeza uwezo wa kijeshi wa umoja huo nchini Libya kupitia operesheni ya baharini ijulikanayo kwa jina la Sophia.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mafunzo na kukiimarisha kikosi cha gadi ya fukwe za bahari cha Libya pamoja na kupambana na magendo ya silaha katika maji ya nchi hiyo, yataongezwa katika majukumu ya operesheni za Sophia.
Umoja wa Ulaya ulianzisha operesheni ya Sophia karibu mwaka mmoja nyuma yaani mwezi Juni 2015 kwa ajili ya kupambana na wimbi la wakimbizi wanaoingia barani Ulaya pamoja na kukabiliana na kanali za magendo ya wanadamu wanaotumia ardhi na maji ya Libya kufanya magendo yao. Nchi 22 za Ulaya zinashiriki kwenye operesheni hiyo.
Tangu alipopinduliwa Kanali Muammar Gaddafi tarehe 20 Oktoba 2012 hadi hivi sasa, Libya haijawahi kushuhudia utulivu wala serikali yenye nguvu ya umoja wa kitaifa, hali ambayo imetoa mwanya kwa makundi ya kigaidi na magenge ya magendo ya wanadamu kufanya mambo yao kwa uhuru nchini humo.