WFP inachunguza wizi wa chakula cha msaada nchini Ethiopia
(last modified Wed, 12 Apr 2023 02:12:29 GMT )
Apr 12, 2023 02:12 UTC
  • WFP inachunguza wizi wa chakula cha msaada nchini Ethiopia

Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) linachunguza wizi wa misaada ya chakula ulioripotiwa katika oparesheni za kibinadamu huko Ethiopia.

Claude Jibidar Mkurugenzi wa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia amesema kuwa shirika hilo limesikitishwa na kuuzwa pakubwa vyakula vya misaada ya kibinadamu katika baadhi ya masoko nchini humo. Amesema jambo hilo linatishia uwezo wa WFP wa kukusanya zaidi misaada kwa ajili ya watu wenye uhitaji. 

Ameongeza kuwa hatua za haraka zinapasa kuchukuliwa ili kukomesha matumizi mabaya ya misaada ya vyakula kwa ajili ya raia walengwa wenye uhitaji huko Ethiopia. 

Missada ya chakula  ya wenye uhitaji Ethiopia yaripotiwa kuibiwa 

Mkurugenzi wa WFP nchini Ethiopia aidha amezitolea wito taasisi washirika wao kupashana taarifa kuhusu vitendo vyovyote vya kutumia vibaya misaada ya kibinadamu na kuuzwa kwake kinyume na ilivyopangwa huko Ethiopia.

Mkurugenzi Mkuu wa WFP nchini Ethiopia hakueleza wazi ni kesi zipi za wizi wa misaada ya chakula iliyojiri huko Ethiopia. Hata hivyo wafanyakazi wawili wa huduma za misaada ya kibinadamu wameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, misaada iliyoibiwa ni pamoja na chakula cha kutosha kuwalisha watu laki moja; ambacho kiligunduliwa kupotea hivi karibuni katika ghala la kuhifadhia vyakula huko Sheraro, mji ambao umeathiriwa pakubwa na mapigano katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.