Jamhuri ya Afrika ya Kati yawalaani wanaotaka kufufua mauaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9619-jamhuri_ya_afrika_ya_kati_yawalaani_wanaotaka_kufufua_mauaji
Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imeyalaani makundi ya watu ambao wanafanya njama za kurejesha ukosefu wa amani na mauaji katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2016 10:03 UTC
  • Jamhuri ya Afrika ya Kati yawalaani wanaotaka kufufua mauaji

Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imeyalaani makundi ya watu ambao wanafanya njama za kurejesha ukosefu wa amani na mauaji katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.

Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Simplice Sarandji, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati akisema kuwa, machafuko yaliyotokea hivi karibuni mjini Bangui na kupelekea watu watatu kuuawa, yamefanywa na watu ambao wana nia ya kuvuruga usalama na kukwamisha kazi za serikali mpya ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amewataka wananchi wa nchi hiyo kuungana na kuwa macho mbele ya maadui wa usalama na utulivu wa nchi yao.

Watu wawili waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa tarehe 11 mwezi huu wa Juni baada ya kuzuka mapigano baina ya Waislamu na Wakristo mjini Bangui.

Siku chache zilizopita pia, kuliokotwa mwili wa Muislamu mmoja katika Eneo la Tatu la Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo Waislamu wamewatuhumu Wakristo kuwa ndio waliofanya mauaji hayo.

Hata hivyo viongozi wa serikali wanasema kuwa, Muislamu huyo ambaye alikuwa ni dereva wa taxi, aliuliwa na majambazi.