Apr 13, 2023 03:29 UTC
  • Wabunge wa Kenya: Wanajeshi watenda jinai wa Uingereza wahukumiwe nchini

Wanajeshi wa Jeshi la Uingereza wanaotoa mafunzo nchini Kenya wanaofanya mauaji nchini humo huenda wakakabiliwa na mashtaka katika mahakama za Kenya iwapo mapendekezo yaliyopendekezwa bungeni na Kamati ya Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni yatapitishwa.

Akizungumzia mapendekezo hayo, mbunge Nelson Koech, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni, amesisitiza kwamba yanalenga kuwawajibisha wale wanaofanya uhalifu katika "ardhi ya Kenya".

Inatarajiwa kuwa marekebisho hayo yataruhusu Kenya kutatua aina zote za matatizo yanayohusisha wanajeshi wa Uingereza ambayo yamesalia katika utata wa kisheria kwa miongo kadhaa.

Nelson Koech, amesema: "Inapasa taifa mwenyeji kuhakikisha kwamba mtu yeyote ambaye tumetia saini naye mkataba anazingatia sheria za nchi. Kesi za mauaji au uharibifu wa mazingira hazingetokea iwapo maafisa wa Kenya wangekuwa wanapata mafunzo nchini Uingereza."

Haya yanajiri huku kukiwa na mjadala mkubwa wa umma kuhusu mauaji ya Agnes Wanjiru yaliyofanywa na mwanajeshi wa Uingereza huko Nanyuki, Kaunti ya Laikipia, zaidi ya miaka kumi iliyopita. Mama huyo aliyekuwa na umri wa miaka 21 aliuawa  Machi 2012. Mwili wake ulipatikana kwenye tanki la maji taka katika Hoteli ya Lions Court huko Nanyuki. Vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kwamba askari  mmoja wa nchi hiyo alikiri kuwa mwenzake alihusika na uhalifu huo.

Maandamano ya kutaka haki itendeke baada ya askari wa Uingereza kumuua Agnes Wanjiri nchini Kenya

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa Kitengo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) kilishindwa kuzingatia sheria za nchi na za kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira. Kando na hayo, wabunge wa Kenya wanapendekeza kwamba wanajeshi wanaofika Kenya kwa ajili ya mazoezi au mafunzo wanapaswa kuheshimu mila na tamaduni za jamii za mashinani na kutoa huduma kwa jamii za maeneo ya mazoezi.

BATUK ni kitengo cha mafunzo kilichoko Nanyuki, Kaunti ya Laikipia, chini ya makubaliano na serikali ya Kenya.

Tags