HRW: Serikali ya Tunisia imedhamiria kukivunja chama cha Kiislamu cha Al-Nahdhah
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limefichua njama zinazopangwa na viongozi wa serikali ya Tunisia za kulivunja na kulisambaratisha kikamilifu Vuguvugu la Kiislamu la An-Nahdhah, ambacho ndicho chama kikubwa zaidi cha siasa nchini humo.
Rashed Al-Ghannoushi, Kiongozi wa chama cha Kiislamu cha An-Nahdhah na mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Kais Saied, alikamatwa katikati ya mwezi Machi, na baada ya hapo ofisi za chama hicho zilifungwa.
Kwa mujibu wa ISNA, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetangaza kuwa, viongozi wa serikali ya Tunisia wameshadidisha hujuma zao dhidi ya wapinzani na kuchukua hatua kwa lengo la kuivunja na kuisambaratisha kikamilifu An-Nahdhah, chama kikubwa zaidi cha siasa nchini humo.
Human Rights Watch imeeleza katika ripoti yake kwamba, serikali ya Tunisia imewakamata takriban wanachama 17 wa sasa na wa zamani wa An-Nahdhah, akiwemo kiongozi wake Rashed Al-Ghannoushi, na imezifunga ofisi zote za chama hicho nchini kote.
Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limebainisha pia katika ripoti yake kwamba, kutiwa nguvuni watu hao kuliendelea kufuatia wimbi la kamatakamata lililoanza mwezi Februari mwaka huu ambalo liliwalenga shakhsia mbalimbali wa kisiasa; na kwamba watu wasiopungua 30 walikamatwa, wengi wao wakituhumiwa kula "njama dhidi ya usalama wa nchi".
Ripoti ya Human Rights Watch imezitaka mamlaka za Tunis ziwaachie huru haraka iwezekanavyo wale wote waliowekwa kizuizini kiholela na kuondoa vizuizi vya uhuru wa kujumuika na kukusanyika.
Salsabil Shelali, mkurugenzi wa masuala ya Tunisia katika shirika la Human Rights Watch, amesema: "baada ya njama za uenezaji hofu na chuki dhidi ya An-Nahdh na kubuni tuhuma nzito zisizo na ushahidi dhidi ya chama hicho kikuu cha upinzani, maafisa wa serikali ya rais Kais Saeid sasa wamechukua hatua inayolenga kukivunja chama hiki".
Aidha, Shelali amebainisha kuwa, mbinu za karibuni za viongozi wa Tunisia zimelenga kutekeleza amri ya kuzima sauti za ukosoaji.
Rais Kais Saeid wa Tunisia amejiongezea mamlaka ya utawala kupitia katiba mpya aliyopitisha nchini humo. Mnamo mwaka 2021 kiongozi huyo alichukua hatua kadhaa zisizo za kawaida ikiwemo kulivunja bunge na taasisi zingine za dola. Wapinzani wake wanasema, alichokifanya kiongozi huyo ni kujiundia utawala wa mtu mmoja.../