Zimbabwe yaomba msaada $ Bilioni 1.5 kukabiliana na njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i973-zimbabwe_yaomba_msaada_bilioni_1.5_kukabiliana_na_njaa
Serikali ya Zimbabwe imetoa ombi la msaada wa dharura wa dola zaidi ya bilioni 1.5 za kimarekani ili kununua nafaka kutoka nchi za nje na kuboresha ukulima nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2016 11:54 UTC
  • Zimbabwe yaomba msaada $ Bilioni 1.5 kukabiliana na njaa

Serikali ya Zimbabwe imetoa ombi la msaada wa dharura wa dola zaidi ya bilioni 1.5 za kimarekani ili kununua nafaka kutoka nchi za nje na kuboresha ukulima nchini humo.

Zimbabwe ambayo pato lake kuu linatokana na kilimo, imekumbwa na ukame wa muda mrefu uliosababishwa na El Nino, ambao unaaminika kuwa mbaya zaidi katika miaka 60 iliyopita nchini humo.

Kufuatia ukosefu wa mvua, mimea imekauka huku mifugo ikiangamia; na wakulima ambao ni asilimia 70 ya watu wote wa Zimbabwe wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuishi.

Makamu wa rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema, serikali ya nchi hiyo inapanga kununua tani milioni 1.4 za nafaka kutoka nchi za nje mwaka huu ili kulisha watu zaidi ya milioni 3 wanaoathiriwa na ukame. Sehemu ya fedha zinazochangiwa zitatumika katika kukarabati mfumo ulioharibika wa umwagiliaji mashamba maji.

Siku ya Jumapili Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alitangaza hali ya maafa kufuatia ukame mkali ulioathiri maeneo mengi ya vijijini nchini humo.

Tangazo hilo linatazamiwa kuitikiwa na jamii ya kimataifa kwa kutolewa misaada ya chakula kwa Zimbabwe. Vijiji vingi vya kusini mwa Zimbabwe vimepoteza mifugo ya ng'ombe na mazao kutokana na ukame mkubwa ulioikumba nchi hiyo. Mabadiliko ya tabia nchi yameziathiri nchi mbalimbali duniani ikiwemo kutokea mafuriko, ukame, joto kali na kadhalika.