Maelfu wakimbia mafuriko Somalia baada ya miezi kadhaa ya ukame mkubwa
Maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao katikati mwa Somalia baada ya Mto Shabelle kuvunja kingo zake huko Beledweyne.
Mvua kubwa iliyoandamana na mafuriko katika eneo hilo imesababisha uharibifu wa miji na vijiji, na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imetahadharisha kuhusu ongezeko la magonjwa kama vile kipindupindu huku miundombinu ya eneo hilo ikiathirika.
Mohamed Yusuf ni mkazi wa eneo la Beledweyne na anasema: "Tulikimbia mafuriko ambayo yameuzamisha mji wetu, watu walikimbilia katika maeneo salama kwa sababu mvua ilinyesha kwa wingi kwa siku nne na kusababisha mafuriko."
Mafuriko yameikumba Somalia baada ya nchi hiyo kuathiriwa na ukame mkubwa kwa miezi kadhaa huku takwimu za kimataifa zikionyesha kuwa idadi ya wakimbizi wa ndani duniani kote imefikia milioni 32.6 kutokana na majanga ya kimaumbile mwaka uliopita.
Hassan Ibrahim Adbulle, Naibu Gavana wa Mkoa wa Hiran huko Somalia ameeleza kuwa, katika baadhi ya mikoa wakazi wake wote wamelazimika kuhama makazi kutokana na mafuriko. Wakazi wengi wa wilaya nne za mji wa Beledweyne wamelazimika kuyahama makazi yao kwa sababu ya mafuriko.
Mafuriko hayo yameikumba Somalia katika hali ambayo miezi kadhaa iliyopita nchi hiyo iliathiriwa na ukame ambao umeua makumi ya maelfu ya watu na kuangamiza mazao na mifugo.