Museveni: Tutalipiza kisasi cha shambulio la al-Shabaab dhidi ya UPDF Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i98112-museveni_tutalipiza_kisasi_cha_shambulio_la_al_shabaab_dhidi_ya_updf_somalia
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo UPDF litatoa jibu kali kufuatia shambulizi la wanamgambo wa al-Shabaab dhidi ya askari walinda amani wa Uganda walioko nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 28, 2023 06:54 UTC
  • Museveni: Tutalipiza kisasi cha shambulio la al-Shabaab dhidi ya UPDF Somalia

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo UPDF litatoa jibu kali kufuatia shambulizi la wanamgambo wa al-Shabaab dhidi ya askari walinda amani wa Uganda walioko nchini Somalia.

Museveni amesema, katika shambulio hilo la Ijumaa iliyopita dhidi ya askari wa UPDF wanaohudumu chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, baadhi ya wanajeshi hawakuwajibika ipasavyo, huku baadhi yao wakiingiwa na woga.

Amesema magaidi wa al-Shabaab waliokuwa wamejifunga mabomu walijiripua, ili kuingia kwa nguvu kwenye kambi hiyo ya kijeshi ya askari wa Uganda katika eneo la Bulo-Mareer.

Rais Museveni amemtaka Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Wilson Mbasu Mbadi kuunda jopo la uchunguzi ili kuweka wazi matukio ya shambulio hilo la Ijumaa, na idadi ya wahanga. Tayari Jenerali Mbadi amewasili Somalia kufuatilia kadhia hiyo.

Ingawaje Museveni, Umoja wa Afrika na Somalia hazijasema chochote kuhusu idadi ya wahanga wa shambulio hilo la Ijumaa, lakini genge la kigaidi la al-Shabaab limedai kuwa liliua wanajeshi zaidi ya 137 kwenye hujuma hiyo ya Ijumaa.

Askari wa Uganda nchini Somalia

ATMIS sasa hivi kina takriban walinda amani 19,000 huko Somalia. Kikosi hicho mwanzoni kilijulikana kama African Union Mission in Somalia (AMISOM), na mara ya kwanza kilitumwa Mogadishu Machi 2007, kikijumuisha wanajeshi wa Uganda. Aprili 2022, jina la kikosi hicho lilibadilishwa na kuwa African Union Transition Mission au ATMIS, kikiwa na nia ya kuondoka nchini humo kufikia Desemba mwaka ujao baada ya wanajeshi wa Somalia kuchukua jukumu la kulinda nchi.

Maelfu ya walinda usalama wa Umoja wa Afrika wameuawa huku mamia wakijeruhiwa nchini Somalia tangu walipoingia nchini huko, mnamo mwaka wa 2007. Tangu 2007, wanajeshi wa AU walioorodheshwa kuuawa ni takriban 4,000.