Jun 01, 2023 12:01 UTC
  • Luteni Jenerali Abdul Rahim Dagalo
    Luteni Jenerali Abdul Rahim Dagalo

Kiongozi nambari mbili wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), Luteni Jenerali Abdul Rahim Dagalo, ametoa wito kwa jeshi la Sudan kufanya uasi dhidi ya kiongozi wake, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan huku nchi za Afrika zikiwasilisha mpango mpya kwa ajili ya kusitisha vita vya ndani nchini Sudan.

Abdul Rahim Dagalo amesema katika hotuba iliyorushwa kwenye mkanda wa video kwamba kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka, Muhammad Hamdan Dagalo, aliyepewa jina la utani "Hamidti", yuko salama na anapigana kwenye mstari wa mbele.

Matamshi haya yanakuja kufuatia mapigano makali yanayoripotiwa kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka katika maeneo kadhaa mjini Khartoum.

Ripota wa televisheni ya Al-Jazeera ameripoti kuwa milipuko mikali imetokea leo asubuhi, huku milio ya silaha nzito ikisikika karibu na mtaa wa Al-Ghaba na eneo la viwanda katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Vilevile kumesikika milipuko mtawalia usiku wa kuamkia leo Alhamisi kusini mwa Omdurman, wakati vitongoji vya kusini mwa Khartoum pia vikiendelea kushambuliwa vikali kwa mizinga.

Khartoum

Wakati huo huo, kama sehemu ya juhudi za kigeni za kutatua mgogoro wa Sudan, Mkurugenzi wa Ofisi ya Umoja wa Afrika, Mohamed El-Hassan Ould Labat, ameiambia Al-Jazeera kwamba mkutano uliofanyika Addis Ababa jana Jumatano, umebuni ramani mpya ya njia ya kutatua mgogoro wa Sudan.

Umoja wa Afrika umesisitiza kuwa, unapinga uingiliaji wa kigeni katika masuala ya Sudan na kwamba, hilo ni jambo lisilokubalika.

Umoja wa Afrika umesisitiza pia katika sehemu nyingine ya taarifa yake hiyo kwamba, mgogoro wa sasa wa Sudan hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa mtutu wa bunduki.