Jun 02, 2023 02:13 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Zaidi ya milioni moja wakimbia mapigano nchini Sudan

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi tangu mapigano yalipozuka nchini Sudan mwezi Aprili mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa ambaye amezimbia duru za habari kwamba, zaidi ya raia milioni 1.2 wamelazimika kuwa wakimbizi tangu yalipoanza mapigano baina ya pande mbili za kijeshi nchini Sudan.

Kadhalika amesema, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linaendelea kutoa msaada wa chakula kwa raia 15,000 katika mji mkuu Khartoum na kwamba, hadi sasa limefanikiwa kuwalisha zaidi ya watu 782,000 wakiwemo wanawake, watoto na wanaume wanaotaabikla kutokana na kushindwa kujidhaminia chakula.

Sudan ilitumbukia katika hali ya mchafukoge baada ya kuzuka mapigano katikati ya mwezi Aprili mwaka huu kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na jenerali Abdel- Fattah al Burhan na Kamanda wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.

Hadi sasa mapigano hayo yameuwa raia wasiopungua 866 na kujeruhi maelfu ya wengine.

Katika upande mwingine Muungano wa Madaktari wa Sudan ulisema kwenye taarifa yake ya Jumapili kwamba, idadi ya vifo vya raia tangu yalipoanza mapigano nchini humo imeongezeka na kufikia watu 866 na majeruhi 3,721.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Afrika umesisitiza kuwa, unapinga uingiliaji wa kigeni katika masuala ya Sudan na kwamba, hilo ni jambo lisilokubalika.

Umoja wa Afrika umesisitiza pia katika sehemu nyingine ya taarifa yake hiyo kwamba, mgogoro wa sasa wa Sudan hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa mtutu wa bunduki.