Ethiopia yapinga tuhuma za maangamizi ya kizazi huko Tigray Magharibi
(last modified Wed, 07 Jun 2023 10:30:17 GMT )
Jun 07, 2023 10:30 UTC
  • Ethiopia yapinga tuhuma za maangamizi ya kizazi huko Tigray Magharibi

Serikali ya Ethiopia imepinga ripoti iliyotolewa na Shirika la Haki za Binadamu la (HRW) iliyodai kuwa kampeni ya maangamizi ya kizazi imefanyika huko Tgray Magharibi licha ya kutiwa saini makubaliano ya amani mwezi Novemba mwaka jana.

Idara ya Habari ya Serikali ya Ethiopia imesema kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai hayo. Serikali ya Ethiopia imesema katika taarifa yake hiyo kwamba: Hatua hii ya upotoshaji ina lengo la kudhoofisha kuishi pamoja kwa amani na kuchochea migogoro baina ya makabila na kuzuia juhudi za kitaifa za kurejesha amani na kufikia mapatano kwa ajili ya Tigray.

Vita vilizuka mwezi Novemba 2020 kwa kuvikutanisha vikosi vya wanamgambo kutoka eneo la Tigray dhidi ya jeshi la shirikisho la Ethiopia na washirika wake. Vita hivyo aidha vilijumuisha pia wapiganaji kutoka nchi jirani ya Eritrea. Mapigano aidha yaliendelea na kuuawa maelfu ya raia, kusababisha mamilioni kuwa wakimbizi na kuwafanya maelfu ya wengine kuathiriwa na njaa. 

Vita vilivyosababisha njaa kwa wakazi wa jimbo ola Tigray, Ethiopia 

Shirika la Haki za Binadamu limetoa ripoti inayosema kuwa, makubaliano ya amani ya mwezi Novemba mwaka jana ya kuhitimisha vita vya miaka miwili huko Tigray kaskazini mwa Ethiopia yameshindwa kukomesha maangamizi ya kizazi katika eneo lililoathiriwa na mzozo magharibi mwa jimbo hilo maarufu kwa jina la Eneo la Magharibi mwa Tigray."