Waliouawa katika miripuko ya mabomu Somalia wakaribia 30
Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na miripuko ya mabomu katika eneo la Lower Shabelle nchini Somalia imeongezeka na kufikia watu 27.
Abdi Ahmed, Mkuu wa Wilaya ya Qoryoley katika eneo la Lowers Shabelle, kusini mwa Somalia amesema watu 27 wakiwemo watoto wadogo wameuawa kwenye miripuko hiyo ya jana, mbali na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa.
Mashuhuda na maafisa wa serikali katika eneo hilo wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema kuwa, mabomu hayo yaliripuka wakati watoto walipokuwa wakicheza nayo.
Naibu Mkuu wa Wilaya ya Qoryoley, Abdi Ahmed Ali ameomba mamlaka husika kuyaondoa mabomu hayo ambayo ambayo yametawanyika katika eneo hilo ili kuepusha maafa zaidi.
Mkazi wa jiji hilo, Ibrahim Hassan, aliyehojiwa na shirika la habari la AFP, amesema kuwa aghalabu ya wahanga wa miripuko hiyo ni watoto wadogo, ambao walikufa papo hapo baada ya mmoja wao kukanyaga kilipuzi karibu na uwanja wa michezo.
Katika hatua nyingine, jeshi la Somalia limefanikiwa kuzima shambulizi la wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika Mkahawa wa Perls, kwenye fukwe za Bahari Hindi.
Magaidi hao waliivamia na kuidhibiti hoteli hiyo ya kifahari iliyoko katika mji mkuu Mogadishu, na ambayo aghalabu ya wateja wake ni maafisa na viongozi wa serikali.
Wanajeshi wa Somalia walifanikiwa kuumaliza mzingiro huo katika kipindi cha saa nne. Kwa mujibu wa Reuters, watu tisa wameuawa katika shambulizi hilo.